2016-01-13 09:11:00

Huruma ni jina na utambulisho wa Mungu!


Huruma ndilo jina na utambulisho wa Mwenyezi Mungu, hivi ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Andrea Tornielli, mwandishi wa habari za gazeti la “La Stampa” na mhariri mkuu wa tovuti ya “Vatican insider” katika kitabu ambacho kimezinduliwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, “Jina la Mungu ni huruma”. Kitabu hiki kimegawanyika katika sura tisa ambazo ni majibu ya maswali 40 aliyoulizwa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, uliozinduliwa hapo tarehe 8 Desemba 2015.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano haya anafanya rejea katika Maandiko Matakatifu, Mafundisho ya Mababa wa Kanisa pamoja na watangulizi wake, yaani Papa mstaafu Benedikto XVI, Mtakatifu Yohane Paulo II, Mtakatifu Yohane XXIII na Mwenyeheri Paulo VI. Kitabu hiki kimechapishwa katika lugha tano na nakala ya kwanza ikawasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni. Kitabu hiki ni matunda ya mahojiano ya kina na majibu muafaka yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko huku akiwahamasisha waamini kutambua udhaifu wao, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu.

Katika sura ya kwanza, Baba Mtakatifu anafafanua sababu msingi zilizomfanya kuitisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu: kwanza kabisa ni sala, tafakari na mafundisho ya viongozi wa Kanisa waliotangulia, kwa kuona kwamba, Kanisa ni sawa na hospitali iliyoko kwenye uwanja wa vita, linapaswa kuwa karibu zaidi na waamini wake ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Kanisa lilikuwa linahitaji muda wa mageuzi katika maisha na utume wake, kwani watu wengi kwa sasa wamepoteza dhana ya dhambi pamoja na kuhisi kwamba, hakuna uwezekano wa kusamahewa dhambi zao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ulimwengu mamboleo umejeruhiwa sana kutokana na magonjwa ya kijamii, yaani umaskini, mipasuko ya kijamii, utumwa mamboleo pamoja na kutopea kwa imani. Kutokana na sababu zote hizi, binadamu anahitaji huruma ya Mungu na kwamba, huruma ni utambulisho wa Mungu ambaye licha ya magumu yanayomsibu na kumwandama mwanadamu, lakini bado anabaki kuwa mwaminifu katika ahadi zake. Waamini wanapaswa kutambua ubaya wa dhambi kama anavyoelezea Nabii Ezekieli, ili kuambata huruma na msamaha wa Mungu, kwa mwamini kutambua dhambi na mapungufu yake.

Hapa Baba Mtakatifu anawaalika Mapadre kujisadaka kwa ajili ya kuwaungamisha waamini wao kwa: Ibada, ari na moyo mkuu. Pale ambapo muungamishaji anashindwa kumwondolea mwamini dhambi zake, pasi walau ampatie baraka, ili kumwonjesha upendo wa Mungu hata kwa mwamini ambaye kutokana na sababu mbali mbali hawezi kupokea Sakramenti za Kanisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, waungamishaji wana dhamana na wajibu nyeti sana, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Mapadre wawe na ujasiri wa kuwasikiliza kwa makini waamini wanaokimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao, kwani kuna baadhi yao wanatambua kwamba, hawawezi kupokea Sakramenti za Kanisa kutokana na vikwazo mbali mbali, lakini wanaweza kupata baraka ya kusonga mbele katika maisha yao ya Kikristo.

Sura ya Pili, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu zawadi na umuhimu wa maungamo. Anakiri kwamba, mwamini anaweza kuomba huruma ya Mungu moja kwa moja bila kupitia kwa viongozi wa Kanisa waliopewa dhamana na kuwaondolea watu dhambi zao. Lakini, Mama Kanisa kwa busara yake, anataka watoto wake kuonesha moyo wa toba kwa kumwendea Padre anayemwakilisha Kristo Yesu katika kiti cha maungamo.

Hii ndiyo njia sahihi ya kuweza kupata huruma ya Mungu ambayo kimsingi ina mwelekeo pia wa kijamii, tayari kuponya madonda, mipasuko na kinzani za kijamii. Waamini wanakwenda kwenye kiti cha huruma ya Mungu si kwa kutaka kuhukumiwa, bali kukutana na hatimaye, kuambata huruma ya Mungu inayoendelea kuusimamisha ulimwengu. Kutokana na mwelekeo huu, maungamo si kama “mashine ya kufulia nguo” wala “chumba cha mateso na udadisi usiokuwa na mashiko” unaofanywa na baadhi ya waungamishaji, hali ambayo inadhalilisha Sakramenti ya Kitubio. Mapadre watoe mashauri kwa unyenyekevu pasi na kuhukumu, wawe tayari kusamahe kwa moyo wote kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo tu vya huruma ya Mungu.

Sura ya tatu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujitambua kwamba wao ni wadhambi, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Hii ni neema ambayo waamini wanapaswa kuiomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu ni kubwa zaidi kuliko hata dhambi zinazotendwa na mwanadamu na kwamba, msamaha wake ni dawa makini dhidi ya dhambi. Mwenyezi Mungu kama iluvyokuwa kwa Baba mwenye huruma daima anawasubiri watoto wake kukimbilia huruma, kwa njia ya toba. Kitendo cha mwamini kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu kinaonesha toba ya ndani, sala inayopaswa kujikita katika unyenyekevu wa moyo badala ya litania ya maneno mengi!

Sura ya nne, Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata Khalifa wa Mtakatifu Petro anahitaji kuonja huruma ya Mungu katika maisha yake, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, pale alipotambua mapungufu yake akaangua kilio! Muungamishaji asiwe ni mtu mwenye kiburi, bali aoneshe unyenyekevu na ukweli wa maisha, kwa kutambua kwamba, hata yeye pia ni mdhambi anahitaji huruma ya Mungu. Muungamishaji ajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini bila kuhukumu, akionesha huruma aliyokuwa nayo Baba mwenye huruma kama anavyosimuliwa na Mwinjili Luka, hiki ni kielelezo makini cha huruma ya Mungu.

Sura ya tano, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linalaani dhambi, lakini linamkumbatia mdhambi anayetambua dhambi zake, tayari kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Kanisa halina budi kusamehe bila kuchoka kama anavyofundisha Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Mwenyezi Mungu yuko radhi kumpokea mwamini anayeonesha moyo wa toba na wongofu wa ndani, tayari kukumbatia na kuambata huruma ya Mungu. Kanisa lipo ili kuwawezesha waamini kukutana na huruma ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema, ili Kanisa liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake, halina budi kutoka kwa kutambua kwamba, Kanisa ni kama hospitali kwenye uwanja wa vita, ambako linakutana na mjeruhi wanaohitaji kusikilizwa, kueleweka, kusamahewa pamoja na kuonjeshwa upendo. Waamini wakaribishwe kwa heshima na taadhima wanapokimbilia huruma ya Mungu, bila kuwanyanyasa wala kuwakejeri.

Sura ya sita, Baba Mtakatifu anapenda kuwaonya waamini wanaodhani kwamba, wanaweza kujiondolea wenyewe dhambi zao kwani tabia kama hii inamchukiza Mwenyezi Mungu na kwamba, ni “ugonjwa wa kiroho” unaopaswa kupewa tiba muafaka. Waamini waoneshe nia ya kutaka kutubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao, hapa watapata tiba kamili bila kujiaminisha kwamba, wanajiweza kwa kila jambo. Binadamu ni mavumbi mbele ya Mungu, kumbe anapaswa kujinyenyekesha, kutubu na kuomba msamaha na huruma ya Mungu. 

Onyo hili si tu kwa waamini walei hata kwa Wakleri na Watawa ambao wanadhani kwamba, kutokana na maisha na utume wao, hawana sababu ya kukimbilia huruma ya Mungu. Waamini watambue kwamba, kama binadamu wataanguka dhambini mara kwa mara, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanasimama na kusonga mbele, wakijitahidi kukimbilia huruma ya Mungu, tayari kuiambata ili iweze kuwaongoza katika maisha yao.

Kwa waamini hata wale ambao jamii inawaona kuwa wamekengeuka kiasi hata cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha kama wale wanaoshabikia ushoga na mifumo ya utamaduni wa kifo. Watu kama hawa wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma kama Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki inavyofundisha. Kabla ya yote hapa kuna binadamu na utu wake, kumbe, hata watu wa namna hii wanapaswa kuungama na kubaki kuwa karibu na Kristo, ili aweze kuwaganga na kuwaponya kutoka katika undani wa maisha yao.

Huruma ya Mungu si dhana ya kufikirika inayoelea kwenye ombwe anasema Baba Mtakatifu Francisko, bali ni sifa kuu ya Mungu na mafundisho ya Kanisa. Yesu alikuja ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na mauti kwa kumjalia maisha ya uzima wa milele. Ni mganga wa kweli anayewatafuta wagonjwa na wala si wenye haki ambao hawahitaji kutubu na kumwongokea Mungu.

Ikumbukwe kwamba, Mungu anataka binadamu wote waokoke. Yesu anataka kuwaendea wote ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu Baba. Hawa ni wadhambi na wote waliotengwa na Jamii, ili aweze kuwaganga na kuwaponya, tayari kuwarudishia hadhi yao kama watoto wateule wa Mungu. Upendo wa Mungu unaowakumbatia wadhambi wakati mwingine unaonekana kuwa ni kashfa mbele ya macho ya binadamu. Yesu anataka kuwaponya na kuwaokoa wale wanaoteseka kiroho na kimwili; tayari kuwaonjesha huruma ya Mungu.

Waamini wanapaswa kushinda kishawishi cha kujiona kuwa ni watakatifu, wenye haki na wateule, bali watambue kwamba, ni wadhambi na wanahitaji kweli huruma na upendo wa Mungu. Hapa Kanisa linapaswa kuwafungulia watu malango ya huruma ya Mungu katika ukweli na uwazi pasi na unafiki. Kanisa lisiwatwishwe watu mizigo mizito, bali liwaonjeshe waamini huruma ya Mungu pasi na kumezwa na malimwengu, uchu wa fedha pengine hata madaraka.

Katika Sura ya Saba, Baba Mtakatifu anasema, Mdhambi anaweza kuvumiliwa lakini fisadi na mla rushwa, hawa ni watu hatari kwani wanatenda dhambi lakini si wepesi kuungama dhambi zao, tayari kujipatanisha na Mungu. Mafisadi na wala rushwa ni watu wanaowatesa na kudhalilisha wananchi wengine; ni wanafiki. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika mafisadi na wala rushwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuanza ukurasa mpya wa maisha yao. Wamwombe Mungu neema ya kuona aibu kwa dhambi walizotenda.

Huruma ni chachu muhimu sana inayoweza kudumisha umoja na udugu kati ya watu na kwamba, haki peke yake haitoshi, bali inapaswa kukamilishwa na fadhila ya huruma na mapendo, kwani Mungu anavuka haki na kwamba, hakuna haki pasi na msamaha. Msamaha ni msingi wa maisha ya jamii inayojikita katika haki na mshikamano na kwamba, huruma inapaswa kumwilishwa katika maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ndiyo maana Kanisa linapinga adhabu ya kifo.

Familia ni shule ya kwanza ya huruma ya Mungu na kwamba hapa wanafamilia wanajifunza kupenda na kupendwa, kusamehe na kusamehewa. Si matarajio yake kuona malango ya magereza yanafunguliwa na wafungwa wote kuachiwa huru hata wale waliotenda makosa makubwa ya jinai. Hapa Baba Mtakatifu anakaza kusema, wafungwa wasaidiwe kutubu, kuongoka na kuanza tena kuandika ukurasa mpya wa maisha yao, wakiwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani.

Katika sura ya nane, Baba Mtakatifu anawakumbusha walimwengu kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda upeo na anataka kuwaonjesha huruma yake isiyokuwa na mipaka. Mwenyezi Mungu kwanza kabisa anaonesha uso wa binadamu na pili uso wa Kimungu. Yesu anamwangalia mwanadamu kutoka katika undani wa maisha yake na wala si kama mpiga picha anayeangalia mambo ya nje. Mwenyezi Mungu anamshirikisha mwanadamu katika maisha na mipango yake, mwaliko kwa walimwengu kuambata huruma ya Mungu ili kushinda kishawishi cha utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Sura ya tisa ambayo ni hitimisho la maswali 40 ambayo Baba Mtakatifu Francisko amejitahidi kuyajibu kwa ufasaha mkubwa, inajikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; mambo msingi yanayomwezesha mwamini kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Huu ndio mwaliko wa Kristo Yesu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanaalikwa kuwapokea na kuwaonjesha huruma na upendo maskini wa kiroho na kimwili; mdhambi aliyejeruhiwa kutoka katika undani wa maisha yake na kwamba, hapa ndipo Wakristo wanapotakiwa kuonesha ushuhuda wa huruma ya Mungu. Waamini wakumbuke kwamba, mwisho wa siku, wote watahukumiwa kutokana na huruma na upendo kwa jirani zao kama anavyosema Mtakatifu Yohane wa Msalaba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.