2016-01-12 10:33:00

Sala ya kuombea Umoja wa Wakristo imetundikwa kwenye mfumo wa digitali


Mpate kuzitangaza fadhili za Mungu ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2016 katika maadhimisho ya Siku kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma, wakati wa kuhitimisha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Maadhimisho ya Mwaka huu yana umuhimu wa pekee kwani ni sehemu ya mchakato wa mwaliko wa kujenga umoja na mshikamano ili Wakristo waweze kushuhudia huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Baraza la Makanisa Ulimwengu, WCC katika maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo, limeandaa vitini ambavyo vinaweza kupatikana kwenye mitandao ya kijamii, ili kuwasaidia waamini kuweza kusali na kutafakari ujumbe huu mahali popote pale watakapokuwa kwa kutumia simu zao za mikononi. Tafakari za mwaka huu katika mtindo wa digitali zinapatikana kwa lugha ya: Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, Kijerumani na Kireno. Waamini wanaweza kusoma na kuwashirikisha wengine utajiri na hazina inayopatikana kutoka katika Neno la Mungu.

Teknolojia ya “Bible App” tayari imekwisha wekwa kwenye vyombo zaidi ya millioni 204 sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, Matoleo ya Biblia 1, 200 katika lugha 800 yamechapishwa kwa mfumo wa digitali, ili kuliwezesha Kanisa kutumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Tafakari za mwaka huu zinaonesha uhusiano mkubwa uliopo kati ya Sakramenti ya Ubatizo, inayomkirimia mwamini fursa ya kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo pamoja Utangazahi wa Habari Njema ya Wokovu.

Wakristo wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha umoja wa Kanisa kama sehemu ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo na Kanisa lake. Teknolojia ya habari itawawezesha Wakristo sehemu mbali mbali za dunia kuweza kusoma na kuwashirikisha ndugu zao utajiri unaofumbatwa katika Neno la Mungu. Tafakari za mwaka huu zinagusa maisha ya mwamini kama mtu binafsi na Jumuiya ya Wakristo inayochangamotishwa kuhakikisha kwamba inaambata umoja, upendo na mshikamano; tayari kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa watu; imani ambayo kwa hakika inapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.