2016-01-12 07:18:00

Ni huduma inayojikita katika ukweli na uwazi; upendo na mshikamano!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema anamshukuru Mungu kwa kumpatia zawadi ya Daraja Takatifu la Upadre pamoja na kumkirimia neema ya kufanya utume wa kidiplomasia ndani ya Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, kwa kuwa kumsaidizi wa karibu sana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ambaye amepewa dhamana na Kristo ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani; kujenga na kuimaraisha umoja na mshikamano wa Kanisa. Anatambua kwamba, huu ni wito unaomwajibisha zaidi, hususan wakati huu familia ya binadamu inapokabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anapenda kukazia kwa namna ya pekee ari na mwamko wa kimissionari ndani ya Kanisa; mchakato wa mageuzi katika miundo mbinu ya Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, ili kweli Kanisa la Kristo liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake katika ukweli na uwazi. Kumbe, kwa namna ya pekee, Katibu mkuu wa Vatican anapaswa kuwa ni shuhuda wa kwanza katika mchakato huu wa mabadiliko yanayotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kujikita katika majadiliano ya ukweli na uwazi, ili kuweza kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, anautekeleza wajibu huu kama neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani si rahisi kuteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Vatican na hivyo kuwa karibu sana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hapa anapaswa kuchangia weledi, hekima na mang’amuzi yake, ili kweli kuonesha na kushuhudia uso wa ukarimu na huruma unaopaswa kuoneshwa na viongozi wa Kanisa, changamoto endelevu inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Parolin anasema, inawezekana kabisa Padre kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Kikasisi sanjari na kuendelea kuwa ni mwanadiplomasia wa Kanisa, dhamana nyeti katika maisha na utume wa Kanisa. Wakati wa majiundo na malezi yake ya Kipadre, moyoni na akili mwake alikuwa na mawazo tofauti kabisa ya kufanya kazi Parokiani au kusaidia majiundo ya majandokasisi seminarini. Alishangazwa alipoambiwa na Askofu wake kwamba, Kanisa lilikuwa linamwomba amsadake kwa ajili ya utume wa diplomasia ya Kanisa.

Katika maisha na utume wake kama Padre na Mwanadiplomasia, ameona kwamba, inawezekana kabisa mamo haya mawili kwenda pamoja. Wakati mwingine, kwa nafasi yake ya Upadre ameweza kuchangia zaidi, kuliko wanadiplomasia wengine wanaojikita zaidi katika siasa. Pengine mchango huu haukuweza kuleta mabadiliko yaliyokusudiwa, lakini lilikuwa ni jambo la muhimu kulizungumza kwa wakati na mazingira yale.

Kwa njia ya huduma ya Kidiplomasia ndani ya Kanisa anachangia kwa namna ya pekee katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii. Wanadiplomasia wa Vatican kadiri inavyowezekana ni viongozi wanaoshiriki pia katika shughuli za kichungaji kwenye Makanisa mahalia kwa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa pamoja na kutembelea Jumuiya za Kikristo. Matukio kama haya anasema Kardinali Parolin, yalikuwa ni sehemu ya maisha yake kama Balozi wa Vatican nchini Venezuela. Anayakumbuka yote haya kwa moyo wa shukrani, anasikitika kuyakosa, lakini anamshukuru Mungu kwa kila jambo.

Kardinali Parolin katika mahojiano haya na Padre Vito Magno wa Radio Vatican anagusia mada mbali mbali zikiwemo kashfa ambazo mara kwa mara zimewakumba na kuwatikisa Wakleri katika maisha na utume wao wa Kikuhani. Useja anasema ni zawadi kubwa kwa Wakleri, lakini inakabiliwa na changamoto nyingi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Useja utaendelea kubaki ni zawadi kubwa isiyokuwa na mbadala kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake na kwamba, Useja si chanzo kikuu cha kashfa ndani ya Kanisa.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, kashfa mbali mbali zinazolikumba Kanisa ni matokeo ya udhaifu wa kibinadamu; ukosefu wa ukomavu katika maisha, wito na utume wa Kikasisi; malezi tenge pamoja na baadhi ya Wakleri kutokuwa na mang’amuzi mapana kuhusu dhana na wajibu wao ndani ya Kanisa. Hapa kuna haja kwa Mama Kanisa kuendelea kuwafunda watoto wake tunu msingi za maisha ya Kipadre na Kitawa; kwa kuimarisha misingi ya maisha ya ndoa na familia; kwa kukazia tunu msingi za kiutu, kiakili, kiroho na kimaadili.

Majiundo haya yanapaswa kuendelezwa hatua kwa hatua katika malezi ya majandokasisi, hadi kufikia kutoa maamuzi magumu katika maisha yake kwa kufuata Wito wa Kikasisi au kuamua kusaidia kulijenga Kanisa la Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa takatifu. Katika miito hii miwili, usafi wa moyo ni jambo la msingi na wala si tu kwa Wakleri na Watawa peke yao! Hata waamini walei wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakita maisha yao katika usafi wa moyo!

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Kardinali Parolin amegusia pia umuhimu kwa Wakleri na waamini katika ujumla wao kukimbilia upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kuna haja pia ya kuendeleza kukazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ili kwa pamoja kugundua na kumwilisha fadhila ya huruma inayopatikana kutoka katika dini mbali mbali duniani.

Mwelekeo huu unapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lengo ni kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu ili kuondokana na misimamo mikali ya kiimani ambayo imepekelea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kushuhudia kwamba, Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo anasema Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.