2016-01-11 14:57:00

Jumuiya ya Kimataifa yalaani majaribio ya silaha za atomic!


Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja, limelaani majaribio ya silaha za atomic yaliyofanywa na Korea ya Kaskazini hivi karibuni, hata kama ukweli wa jaribio hili bado uko mashakani, lakini Jumuiya ya Kimataifa imelaani kwa nguvu zote kwani hiki ni kitendo kinacho hatarisha amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataufa. Majaribio haya linasema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kinyume kabisa cha taratibu na kanuni zilizowekwa na kwamba, kwa sasa Umoja wa Mataifa utaanza kufikiria ni hatua gani zaidi zichukuliwe ili kuhakikisha kwamba, amani na usalama vinalindwa na kudumishwa.

Hivi karibuni, Rais Kim Jong wa Korea ya Kaskazini ilisikika ikijigamba kwamba, imefanikiwa kufanya majaribio ya silaha za Atomic, ili kujihami na mashambulizi yanayoweza kufanywa na Marekani. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon ameonesha kusikitishwa sana na majaribio haya yanayotishia amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Korea ya Kaskazini inapaswa kuheshimu mpango wa Jumuiya ya Kimataifa unaoitaka kuachana kabisa na majaribio ya silaha za Atomic. Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani amezungumza na viongozi wakuu wa Korea ya Kusini na Japan na kuwahakikishia kwamba, Marekani itaendelea kuwa mstari wa mbele kulinda na kuimarisha amani na usalama katika eneo lao!

Kwa upande wao, viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Korea ya Kusini wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwani kwa sasa nchi yao inakabiliwa na hali ngumu, majaribio ya silaha za Atomic hayatasaidia kurejesha amani na utulivu kati ya watu na badala yake viongozi wa kisiasa nchini Korea ya Kaskazini wanapaswa kujikita katika majadiliano ya kisiasa. Silaha za Atomic ni moto wa kuotea mbali na wala si jambo la kufanyiwa mchezo kwani ni hatari kwa maisha, usalama na maendeleo ya wengi.

Viongozi wa Kanisa nchini Korea ya Kaskazini wanasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi kwa Familia ya Mungu nchini humo kuambata toba na wongofu wa ndani kwa kujikita katika ukweli na uwazi; ili kujenga na kuimarisha umoja na upatanisho kati ya Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini, kwani wote ni ndugu wamoja. Mchakato wa amani Korea ya Kaskazini wanasema viongozi wa Kanisa ni mgumu, pengine kwa njia ya sala, viongozi wa kisiasa wanaweza kufungua milango ya akili na mioyo yao tayari kumpatia nafasi, Yesu Mfalme wa amani aweze kuingia na kurekebisha mambo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.