2016-01-10 13:46:00

Shuhudieni Ubatizo wenu kwa kuishi kikamilifu Ukristo wenu!


Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana ni mwaliko kwa waamini kufanya kumbu kumbu endelevu ya Ubatizo wao pamoja na kuendelea kuwaombea watoto wote waliobatizwa katika siku kuu hii, ili imani waliyorithishwa na wazazi wao iweze kukua na kudumu. Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Mwinjili Luka anaonesha Ufunuo wa Mungu kuwa ni kiini cha tukio hili, wakati Yesu alipokuwa anabatizwa Mtoni Yordani. Sauti ikasikika ikisema, huyu ni mwanangu mpendwa wangu ninayependezwa naye. Hapa Mwenyezi Mungu anamdhihirisha na kumtambulisha Yesu kuwa ni Masiha na Mkombozi wa dunia.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Jumapili tarehe 10 Januari 2016Siku kuu ambayo kwa mwaka huu inajikita kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hapa kuna mwelekeo mpya kutoka katika Ubatizo uliotolewa na Yohane Mbatizaji aliyebatiza kwa maji, lakini sasa Ubatizo unafanyika kwa Maji na Roho Mtakatifu anayeunguza dhambi ya asili na kumkirimia Mbatizwa ile neema ya utakaso.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Roho Mtakatifu anamwokoa mwamini kutoka katika giza la dhambi  na kumwongoza katika utawala wa mwanga unaojikita katika mapendo, ukweli na amani. Wabatizwa wanapokea utu mpya na kuanza kutembea katika upendo wa Mungu kwa vile wamefanyika kuwa ni wana wateule wa Mungu. Hii ni dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa na Wakristo kwa kumfuasa Kristo, Mtumishi mwaminifu, ili wao pia waweze kuwa ni wanyenyekevu, wapole na wenye huruma.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, pengine si rahisi kwa waamini kumwilisha fadhila hizi kutokana na ukweli kwamba, wanazungukwa na hali ya kutovumiliana, kiburi na ugumu wa mioyo. Lakini kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetoka juu, yote haya yanawezekana. Kwa mara ya kwanza wakristo wanampokea Roho Mtakatifu kwa njia ya Ubatizo na kufungua mioyo yao ili kuambata ukweli wote, tayari kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha, upendo na mshikamano kwa ndugu zao.

Roho Mtakatifu anawakirimia waamini huruma ya Mungu na kuwafunika kwa nguvu ya huruma ya Mungu. Roho Mtakatifu anaendelea kuliuhisha na kulitegemeza Kanisa; anasalina pamoja na kuwashirikisha waamini ile furaha ya maisha ya kiroho. Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana ni siku maalum ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Ubatizo, mwaliko wa kumwabata Kristo kwa kutekeleza dhamana ya kuishi kikamilifu kama Wakristo, wanajumuiya wa Kanisa na utu mpya ambao wote wanatambuana kama ndugu.

Wakristo wanapokea Ubatizo mara moja tu katika maisha yao, lakini wanapaswa kuushuhudia kwa njia ya maisha mapya na mwanga wa kuwashirikisha wengine hasa wale wanaoishi katika hali ngumu na kutengwa na jamii kama ilivyokuwa kwa wagonjwa wa ukoma. Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria alikuwa ni mwanafunzi wa kwanza wa Mwanaye mpendwa Yesu Kristo, awasaidie Wakristo kuishi kikamilifu ile furaha na ari ya Ubatizo wao, kwa kuendelea kupokea kila siku, zawadi ya Roho Mtakatifu, inayowafanya kuwa kweli ni Watoto wateule wa Mungu.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka na kuwabariki watoto wote waliobatizwa katika Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana,  na wale ambao wamebatizwa hivi karibuni kutoka sehemu mbali mbali za dunia, bila kuwasahau vijana na watu wazima waliobatizwa hivi karibuni, ili waweze kuongozwa na neema ya Mungu pamoja na kuwasaidia wakatekumeni wote kujiandaa vyema ili kupokea Sakramenti ya Ubatizo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.