2016-01-10 11:16:00

Shemasi Mushobolozi adondosha chozi la shukrani!


Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Kanisa linashangilia ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi kwa kuonesha mshikamano wa dhati na binadamu, ili kumwonjesha huruma na upendo wa Mungu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kupitia katika Lango la huruma ya Mungu ili kuonja na kutambua kwamba, Mungu anawapenda na kuwasamehe watu wake dhambi zao, wakimkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani.

Waamini kama Jumuiya wanahamasishwa kupitia katika Lango la huruma ya Mungu na hii ni changamoto pevu kwa viongozi wa Kanisa wanaotekeleza dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu. Wakleri yaani: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu watambue kwamba, wamechaguliwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na wanapaswa kubaki kati ya watu, ili waweze kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza.

Hii ndiyo furaha ambayo Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari alipenda kuwaonjesha Watu wa Mungu wakati alipokuwa anatoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa Frt.  Danstan Mushobolozi Balayangaki wa Shirika la Consolata, katika makesha ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana hapo tarehe 9 Januari 2016 kwenye Parokia ya "SS. Crocifiso" iliyopo Jimbo kuu la Roma.

Ibada hii ya Ushemasi imehudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka Afrika Mashariki kwani wito na ufuasi wa Kristo unapata chimbuko lake katika maisha ya Kijumuiya na kushuhudiwa na wanajumuiya, vinginevyo, mtu atajitafuta na kubaki katika upweke wake! Askofu mkuu Rugambwa anaendelea kufafanua kwamba, huu ndio ule muda uliokubalika kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili kuweza kusafishwa na kusamehewa dhambi, kwa kutambua kwamba, wamekombolewa si kutokana na matendo yao ya haki, bali ni kutokana na huruma na upendo wa Mungu.

Askofu mkuu Rugambwa amemtaka Shemasi Danstan Mushobolozi kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zake katika upendo, ukarimu , huduma na unyenyekevu, daima akionesha moyo wa shukrani, kutoka kwa Mungu ambaye amemkirimia mambo mengi na makubwa katika maisha. Daima akumbuke kwamba, yeye ni Shemasi asiyekuwa na faida, bali anatumwa ulimwenguni kama  ilivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji ili kumtayarishia Bwana njia si tu kwa maneno, lakini hasa kwa njia ushuhuda wa maisha yenye mshiko na mguso; kwa uaminifu na udumifu, ili kuzima kiu ya matarajio ya watu wa Mungu kwa nyakati hizi.

Shemasi Mushobolozi ametakiwa kuyasadaka maisha yake, tayari kutoka kimasomaso kuwahudumia Kondoo wasiokuwa na mchungaji, kwa kuwaonesha watu dira na njia ya kufuata, bila kuchoka wala kukata tamaa, daima akijihitahidi kuambata tunu msingi za Kiinjili na kwenda mahali popote pale ambapo Shirika litamtuma kwenda. Aoneshe upendo na ukarimu kwa wale wote atakaokutana nao katika maisha na utume wake sanjari na kushuhudia Injili ya furaha bila kuwa na makunyanzi moyoni!

Askofu mkuu Rugambwa amemtaka Shemasi Mushobolozi kumezwa na upendo wa Mungu, unaosafisha na kupyaisha; ni changamoto ya kuzama katika Ubatizo wa huruma ya Mungu kwa kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani. Atambue kwamba, maisha na wito aliojichagulia una raha na karaha zake; una utamu na shida zake, lakini jambo la msingi ni kukuza na kudumisha udugu na ufuasi wa Kristo, kwa kushuhudia majiundo na malezi makini; ushuhuda na furaha ya wale wote aliokutana nao katika hija ya maisha yake, ili aweze kuwa kweli ni mtumishi mwaminifu, kwa kujimwaga bila ya kujibakiza, kama ilivyokuwa kwa Yesu alipogeuza mikate mitano na samaki wawili, watu wakala na kushiba. Shemasi Mushobolozi anatakiwa kujenga utamaduni wa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari na Sakramenti za Kanisa; kwani hii ni hazina inayoweza kuwashangaza wengi watakapokutana naye katika maisha na utume wake kama Shemasi na hatimaye, Padre.

Mara baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Shemasi Danstan Mushobolozi Balanyangaki alitokwa na chozi la shukrani kwa Mungu, Familia, Kanisa na Shirika la Waconsolata waliompokea, wakamlea na kumtunza hadi kufikia hatua hii ya kupewa Daraja Takatifu la Ushemasi wa mpito. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kumsindikiza katika hija ya maisha na wito wake, ili kweli aweze kuwa ni chombo cha faraja, upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake.

Itakumbukwa kwamba,  Shemasi Danstan Mushobolozi Balayangaki aliweka nadhiri za daima kwenye Shirika la Wamissionari wa Consolata, hapo tarehe 8 Januari 2016. Ibada ya nadhiri za daima iliongozwa na Padre Michelangelo Piovano, Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Consolata, Kanda ya Italia aliyemtaka Danstan kujikita katika upendo, huruma na umoja katika maisha na utume wake kama Mmissionari wa Consolata.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.