2016-01-10 11:06:00

Imani ni urithi mkubwa unaoweza kutolewa na wazazi kwa watoto wao!


Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, Lango la huruma ya Mungu na uzima katika Roho; ni mlango unaomwezesha mwamini kupata Sakramenti nyingine za Kanisa. Kwa njia ya Ubatizo, mwamini anaokolewa kutoka katika dhambi na hivyo kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo waamini wanafanyika kuwa kweli ni watoto wa Mungu na viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kwa Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanajishiriki ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo, tayari.

Watoto wachanga kwa vile wanazaliwa na hali ya kibinadamu iliyoanguka na kuchafuliwa na dhambi ya asili, hata watoto wachanga wanalazima ya kuzaliwa upya katika Ubatizo, ili wawekwe huru na nguvu za giza na kuingizwa katika utawala wa uhuru wa watoto wa Mungu, ambamo watu wote wameitwa, kwani wokovu ni kipaji kinachotolewa bure na hudhihirika kwa namna ya pekee katika Ubatizo wa watoto wachanga. Hapa wazazi na walezi wa watoto hawa wanatambua  kwa dhati kabisa umuhimu wa kulea uzima mpya ambao Mwenyezi Mungu amewaaminisha.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, Jumapili tarehe 10 januari 2016 Sherehe ambayo inafunga rasmi kipindi cha Noeli na kuanza kipindi cha Mwaka wa Kanisa, ametoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga 26 na kati yao kuna wavulana kumi na watatu na wasichana kumi na watatu katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kikanisa cha Sistina, kilichoko hapa mjini Vatican. Hiki ni kipindi cha siku arobaini tangu Mtoto Yesu alipozaliwa. Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu wanampeleka Mtoto wao Hekaluni ili kumtoa sadaka kwa Mungu.

Baba Mtakatifu amewaambia wazazi na wasimamizi wa watoto waliobatizwa kwamba wamewapeleka watoto wao ili kubatizwa na kwa njia hii, kuwarithisha imani ya Kanisa ambayo imerithishwa ndani ya Kanisa na vizazi baada ya vizazi, kiasi kwamba, imani inakuwa kama mtandao unaowagusa watu wengi zaidi. Watoto hawa baada ya muda, wataweza kuchukua nafasi za wazazi wao, wakiwa na watoto wao wenyewe na wao pia watawaombea zawadi ya imani kutoka kwa Mama Kanisa, Imani ambayo inapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo kwa kulipokea Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anawataka wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanalinda na kudumisha imani ya watoto wao, urithi mkubwa ambao mzazi anaweza kumwachia mtoto wake hapa duniani. Wazazi wawe makini ili kuhakikisha kwamba imani hii inatunzwa na kukuzwa, ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Baba Mtakatifu amewahakikishia akina mama wanaonyonyesha kuwapatia watoto wao chakula pale wanaposikia njaa, Kanisani wako huru kabisa pasi na mashaka. Mwishoni, baba Mtakatifu amewaalika wazazi na walezi wa watoto waliobatizwa kumwinulia Mwenyezi Mungu, chemchemi ya maisha mapya, sala zao kwa ajili ya watoto hawa ambao wameitwa kuwa ni wateule wa Kristo Yesu, kwa ajili ya wazazi na wasimamizi wao wa Ubatizo pamoja na Wakristo wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.