2016-01-09 06:44:00

Onesheni huruma na upendo kwa maskini zaidi!


Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa Familia ya Mungu nchini Ufilippini kupiga magoti, ili kuonesha fadhila ya unyenyekevu kwa maskini na wote wanaoteseka kutokana na umaskini wa hali ya kipato! Iwe ni fursa ya kuwaonjesha wengine huruma ya upendo wa Mungu, wale wote waliojeruhiwa kutokana na dhambi. Hii ni changamoto kwa Familia ya Mungu nchini Ufilippini kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini wakati huu Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Kongamano la Ekaristi Takatifu kimataifa, litakalofanyika Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini, mwezi Januri, 2016. Ni mwaka wa Familia kwa familia ya Mungu nchini Ufilippini. Matukio yote haya yasaidie kuimarisha imani, matumaini, mapendo, lakini zaidi huruma ya Mungu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha huruma na mapendo; toba na wongofu wa ndani dhidi ya utamaduni na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Waamini wawe na ujasiri wa kutoa na kupokea huruma na msamaha kutoka kwa wengine. Maaskofu wanawataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa familia kusali na kushiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, ili kupata rehema na neema katika maisha ya kiroho.

Maaskofu wanapenda kuonesha masikitiko yao kwa familia nyingi nchini Ufilippini zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha. Wanawataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa Ekaristi Takatifu kwa kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengine. Waamini wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa kuhudumiana wao kwa wao kama alivyofanya Yesu kwa kuwaosha miguu mitume wake, ile siku iliyotangulia kuteswa kwake, changamoto endelevu ya huduma ya mapendo kwa waamini wote, lakini kwa namna ya pekee wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. 

Mwaka huu iwe ni fursa ya kumwilisha muujiza wa upendo ndani ya familia kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, kielelezo cha imani tendaji. Familia inayofumbata maisha ya sala, itaendelea kushikamana katika umoja, itaonesha ujana wa maisha na kuendelea kujipyaisha daima kutokana na nguvu ya maisha ya kiroho iliyomo ndani mwao! Kumbe, maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu uwe ni mwaka wa huruma na maisha ya sala, umoja na mshikamano wa upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.