2016-01-09 07:32:00

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Moto wa kuotea mbali!


Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya anasema, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko aliwaalika waamini kupitia kwenye Lango la huruma ya Mungu, ili kugundua ukuu wa huruma na upendo wa Mungu unaotolewa kwa kila mwamini. Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuwatafuta waja wake, tayari kuwakumbatia na kuwaonjesha huruma na mapendo yake ya kibaba. Mwaka wa huruma ya Mungu ni nafasi ya pekee kuonja na kuwagawia wengine huruma ya Baba.

Baba Mtakatifu alisema, mwamini anapopita kwenye Lango la huruma ya Mungu anapaswa kujisikia kwamba anashirikishwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la huruma, upendo na upole wa Mungu. Hapa waamini wanahimizwa kuondokana na woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko wala mvuto katika maisha yao ya kila siku, kwani waamini wanataka kuishi na kumwilisha ile furaha inayobubujika ndani mwao kwa kukutana na Kristo Yesu; tayari kufanya mabadiliko katika maisha ya kiroho kwa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Askofu mkuu Rino Fisichella anasema, uzinduzi wa Lango la huruma ya Mungu ulifanywa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika, alipofungua Lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Baba Mtakatifu alitaka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Bara la Afrika kutambua uwezo na mchango wake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu kwa sasa na kwa wakati ujao!

Ni utashi wa Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu liwe ni tukio la Kanisa zima, kwa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia kushiriki kikamilifu kadiri ya nafasi na mazingira yao, ili kila mwamini aweze kutambua na kuguswa na ile nguvu ya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, kweli anakuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa watu wanaomzunguka.

Askofu mkuu Rino Fisichella anakaza kusema, tangu kuzinduliwa kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, shuhuda kutoka sehemu mbali mbali za dunia zinaonesha kwamba, waamini wameguswa na kupokea ujumbe huu kwa imani na matumaini makubwa. Kuna umati mkubwa wa familia ya Mungu unaoendelea kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Kwa hakika haya ni matendo makuu ya huruma ya Mungu kwa waja wake!

Hii ni changamoto kubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajikita kwa namna ya pekee katika wito na maisha ya kimissionari kwa kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji! Imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya siku! Kuna mamillioni ya watu wanaosubiri kusikia Injili ya furaha ikitangazwa masikioni na mioyoni mwao, tayari kumfuasa Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia, ili kuonja huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yaguse maisha ya mwamini binafsi, ili kuona hamu ya kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Ni changamoto ya kuanza ukurasa mpya wa maisha kwa kushikamana na Kristo Yesu. Roma inaendelea kuwa ni kiini cha maadhimisho haya kutokana uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa. Kumekuwepo na idadi kubwa ya waamini na mahujaji waliofika mjini Roma ili kushiriki katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na matukio ya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia, hali ambayo imewafanya baadhi ya waamini kusita kushiriki katika matukio makubwa makubwa kwa hofu ya usalama wa maisha yao! Mjini Roma ulinzi na usalama anasema Askofu mkuu Rino Fisichella umeimarishwa na waamini wanaweza kushiriki kikamilifu pasi na wasi wasi wowote. Kila siku kuna vikundi vya waamini wanaofanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Lango la huruma ya Mungu, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, huku wakiwa wamebeba Msalaba wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huu ni ushuhuda wa imani inayogusa na kuleta mabadiliko katika maisha ya watu!

Huruma ya Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko ni shirikishi, inayomwambata kila mtu, ili baadaye, aweze kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma hii kwa jirani na wote anaokutana nao katika viunga vya maisha yake. Huruma ya Mungu ni kiini cha Fumbo la Upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Waamini wanaendelea kuhamasishwa kushiriki katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma, ili huruma na upendo wa Mungu viguse akili na mioyo ya watu, tayari kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.