2016-01-09 08:32:00

Msifumbie macho mauaji, nyanyaso na dhuluma dhidi ya Wakristo!


Kardinali Donald William Wuerl, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Washington DC, Marekani katika tafakari yake kuhusu mauaji, nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa Wakristo zaidi ya millioni mia mbili sehemu mbali mbali za dunia anasema, hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda ambao Wakristo wanaoutoa kwa Kristo na Kanisa lake katika ulimwengu mamboleo. Kuna baadhi ya nchi kuwa Mkristo inaonekana kana kwamba, ni kosa la jiani, hali ambayo imepelekea kuibuka kwa mashuhuda wa imani sehemu mbali mbali za dunia, watu wanaosadaka maisha yao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani yao.

Takwimu zinaonesha kwamba, Wakristo zaidi ya millioni mia mbilia kutoka katika nchi 60 dunia wanaendelea kuuwawa, kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo. Madhulumu haya ni matokeo ya misimamo mikali ya kidini na kiimani inayosababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Kuna baadhi ya Wakristo wanabambikizwa kesi za kufuru dhidi ya dini nyingine, ili wakione cha mtema kuni. Lakini kuna mauaji yanayoendelea kutoa hukoIraq, Syria, Nigeria, Pakistan, India, Sudan, Korea ya Kaskazini na katika nchi nyingine ambako mauaji haya yanatendeka pengine hata kwa usiri mkubwa!

Kardinali Donald William Wuerl anasikitika kusema, matukio yote haya hayapewi kipaumbele cha pekee na wanadiplomasia au wanasiasa kwa kisingizio kwamba, haya ni masuala ya kiimani. Wakristo wanaoteseka wanaonesha uvumilivu mkubwa kiasi cha kushindwa kushtua dhamiri za wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa ili  kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea dhidi ya mauaji na nyanyaso wanazokumbana nazo! Lakini Jumuiya ya Kimataifa inakumbushwa kwamba, mauaji, nyanyaso na dhuluma dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni matukio ambayo yanakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, hususan uhuru wa kuabudu.

Kardinali Wuerl anakaza kusema, Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo wote kuonesha mshikamano wa Uekumene wa damu, ili kwa pamoja waweze kupaaza sauti zao dhidi ya mauaji na nyanyaso wanazokabiliana nazo! Waamini waseme ili kuvunja ukimya na hali ya kutojali inayopelekea maelfu ya wakristo kuendelea kupoteza maisha yao. Kutokana na msimamo huu, Kardinali Wuerl ameamua kuandika kitabu kama kielelezo cha mshikamano na Wakristo wanaodhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mshikamano ni kiungo muhimu sana cha umoja ndani ya Kanisa la Kristo Yesu.

Mshikamano na majadiliano ya kiekumene unawawezesha Wakristo kushirikishana tunu msingi za maisha na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwani wote wanajisikia kuwa ni sehemu ya viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani, Kanisa. Mashuhuda wa imani wanapoteseka na kunyanyasika, waamini wengine pia wanateseka na kunyanyasika pamoja nao! Kifo dini ni sehemu ya vinasaba, maisha na utume wa Kanisa tangu mwanzo kabisa na daima mashuhuda wa imani wataendelea kuibuka ndani ya Kanisa kila kukicha kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo Mwana wa Mungu ameonesha huruma na upendo wake kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, pale alipoyamimina maisha yake pale Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ushuhuda wa imani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake, kwa njia hii Wakristo kwa namna ya pekee wanafanana na Kristo. 

Kifodini ni zawadi ya imani ambayo inawambata waamini wote, lakini ni wachache tu wanaoweza kuipokea zawadi hii kwa imani na matumaini kwa kuonesha ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake mbele ya watesi wao pasi na mashaka wala woga wowote! Njia ya Msalaba ni sehemu ya Kanisa, lakini Wakristo pia wanayo haki na kuheshimiwa na kuhakikishiwa uhuru wa kuabudu ambao ni nguzo ya haki msingi za binadamu. Ukosefu wa haki msingi za binadamu ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Umefika wakati kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu pamoja na kupinga misimamo mikali ya kidini inayosababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia sehemu mbali mbali za dunia Uhuru wa kuabudu ni haki ya kila mwananchi na wala haupaswi kuwa ni upendeleo kwa watu wachache tu ndani ya Jamii.

Kardinali Donald William Wuerl anasema kwa moyo mkuu kabisa kwamba, inafurahisha na kupendeza kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu; Kuabudu Fumbo la Utatu Mtakatifu na kutangaza kwa nguvu zote kwamba, Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kiini cha imani ya Kikristo ambayo Kanisa linaona fahari kuitangaza na kuiungama mbele ya walimwengu. Waamini wanahitaji haki, amani na usalama, ili kuweza kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa moyo wa utulivu pasi na woga wala mashaka ya kushambuliwa kwa sababu yoyote ile!

Mashambulizi ya kigaidi sasa ni wasi wasi wa kimataifa, kwani yanapotokea hayachagui wala kubagua, kumbe, kuna haja ya kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaalikwa kwa namna ya pekee kuonesha upendo na mshikamano na mashuhuda wa imani wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mababa wa Kanisa daima wamekumbusha kwamba, damu ya wakristo ni mbegu ya Ukristo na maendeleo ya Kanisa. Pale ambapo Kanisa limepitia vipindi vigumu vya maisha na utume wake, hapo imani imeimarika na Wakristo wengi wamekuwa ni mashuhuda kweli kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.