2016-01-09 10:21:00

"Huu si upendo, bali mahaba ya Mungu kwa binadamu" Yaani we acha tu!


Wapendanao hususani wachumba, wanavutiwa na mambo mbalimbali wayaonayo kwa wapendwa wao. Wengi wanavutiwa na uzuri wa uso hadi wanasema: “reception imekubali.” Uso  ni alama ya nje  inayoonekana na kuvutia macho hadi kupenda. Zipo alama tatu za nje yaani aina tatu za uso – reception – wa Mungu uliyojidhihirisha katika Yesu na kuonekana machoni kwa watu hadi wakavutika kumfuata. Kuonekana kwa nyuso hizo ndiko kunakoitwa Epifania au tokeo la Bwana. Epifania ya kwanza ndiyo ile tuliyosherekea tarehe 6 Januari alama yake ya nje ni nyota au mwanga uliowaongoza Majusi toka Mashariki hadi Betlehemu pangoni pahala alipolala Mtoto Yesu. Epifania ya Majusi iliwakilisha mwanga wa uso wa Mungu ambayo wapagani walitafakari kuhusu mwumbaji aliyeumba yote.

Halafu Epifania ya Arusi ya Kana, na alama yake ni divai yenye maana ya furaha, “majichano” na mashangilio yanayomwonesha Mungu kuwa Bwana Arusi “aliyemzimikia binadamu” kwa mahaba. Mungu anampenda sana binadamu na anamtakia awe na furaha tele moyoni na akilini mwake. Divai yenye kuchangamsha ndiyo sura ya pili ya Mungu kama tunavyosali baada ya komunio: “Damu Azizi ya Kristo (divai) inichangamshe au inilevye.”

Kisha kuna Epifania ya uso wa Mungu katika ubatizo wa Yesu tunaosherekea leo. Antifona mbili kwa wimbo wa Zakaria na Wimbo wa Bikira Maria zina maneno yanayounganisha Epifania hizi tatu pamoja: “Leo Kanisa limeunganika na Bwana arusi wake wa mbinguni, maana Kristo amelitakasa na dhambi zake katika mto Yordani: Mamajusi wanafanya haraka kwenda kwenye arusi hiyo ya kifalme, na hutoa zawadi: wageni hufurahi kwa kuwa Kristo amegeuza maji yawe divai, aleluya” (Wimbo wa Zakari, unaimbwa sikukuu ya Epifania Tokeo la Bwana na Wimbo wa Bikira Maria katika Masifu ya pili ya Jioni). Wimbo ufuatao wa Antifona kwa Bikira Maria unaimbwa sikukuu ya Ubatizo wa Bwana Masifu ya pili: “Maajabu matatu yanaipambanua sikukuu hii tunayoadhimisha: leo nyota iliwaongoza Mamajusi kwenye hori; leo maji yaligeuzwa kuwa divai arusini Kana; leo Kristo alitamani kubatizwa na Yohane katika mto Yordani ili kutuletea wokovu, aleluya.”

Injili ya leo inaanza hivi: “Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote waliwazawaza mioyoni mwao habari za Yohane kama labda yeye ndiye Kristo.” Kungoja kunakosemwa hapa ni kwa kimasiha. Kwa karne nyingi taifa la Israeli lilingoja na na kusadiki kwamba Mungu ni mwaminifu na ataitekeleza ahadi aliyoitoa kwa Waisraeli. Kwa hiyo watu walikuwa bado wanangoja kutimilizwa kwa ulimwengu mpya, ulimwengu wa haki na upendo. Hatimaye, Yohane Mbatizaji alionesha cheche fulani za kukamilika kwa ahadi hiyo jinsi alivyofanya vizuri mambo yake hadi wote wakakiri kwamba alikuwa nabii mwema. Lakini ubatizo wake ulimtakasa mtu kwa nje, yaani ulikuwa alama ya nje ya kumwongokea Mungu. 

Watu walipomwuliza endapo yeye ndiye Kristo wanayemngoja akakataa na kusema:“Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.” Yohane aliwaandaa watu kuupokea ubatizo halisi wa ulimwengu utokao juu. Alikiri pia kwamba maji yanafaa kuosha mwili kwa nje lakini inabidi maji hayo yaingie ndani kumsafisha na kumbadilisha mtu kama maji yale ya yule mwanamke msamaria kwenye kisima cha Yakobo alipomwomba Yesu: “Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu wala nisije hapa kuteka.” (Yoh 4:15).

Ubatizo wa moto ni ule unaomwunguza mtu wa ulimwengu wa kale (mnyama wa kale) na kumbadilisha kuwa mtu mwema wa ulimwengu mpya. Epifania iliyokuwa katika ubatizo iliwahusu watu wote kama isemavyo: “Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa” Kumbe alipoingia Yesu kubatizwa wakaja pia wakosefu wengi wakichangamana ili kubatizwa pamoja naye. Kwa hiyo Yesu anajilinganisha na wadhambi, anawapenda na anaingia nao kubatizwa. Kumbe Waisraeli (Wayahudi) walimngojea na kumtegemea Mungu mwenye mamlaka ya hali ya juu, atayewakandamiza maadui. Epifania hii ndiyo inayoendeleza mipango ya Mungu kwa binadamu, yaani upendo. Mungu aliongoza watu wake kwa moto jangwani na sasa anawapa roho yake.

Epifania ya Mungu tunayoiona katika ubatizo wa Yesu ni mwendelezo wa Epifania ya Mungu aliyekuwa anatembea pamoja na watu wake katika Agano la kale. Hii ndiyo Epifania iliyoko katika imani ya mkristu. Epifania hii inatofautina na ufunuo wa dini nyingine zote zilizoko duniani kuwa Mungu anaweza kuishi pamoja na watu wake na kutembea nao. “Ikawa watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba,” (Lk 3:21) yaani, baada ya kubatizwa Yesu alibaki anasali, kuonesha kwamba alikuwa katika mahusiano ya moja kwa moja na Mungu.

Kisha “mbingu zilifunguka.” Kumbe Mungu alishafunga mbingu kutokana na maovu ya watu, na sasa mbingu zimefunguka. Hapa tunaona Epifania ya sala zinazowezesha mbingu kufunguka na Mungu kutufikia. Kwa hiyo mbingu hazitafungwa tena kwani Mungu yuko pamoja nasi. Hii ndiyo Epifania ya uso wa Mungu inayong’aa katika ubatizo wa Yesu. Baada ya kufunguka mbingu: “Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili kama hua.” Picha ya hua (njiwa) tunaiona pia katika kitabu cha Mwanzo Noa, aliporusha njiwa alama ya mwisho wa gharika na mwanzo wa ulimwengu mpya, kwamba sasa kuna amani na mahusiano mapya kati ya anga na dunia. Kadhalika hua aliyemshukia Yesu ni alama inayoonesha mwisho wa ulimwengu wa kale na mwanzo wa ulimwengu mpya, na kwamba sasa kuna amani na mahusiano mapya kati ya mbingu na dunia. 

Kushuka kwa Roho kutoka mbinguni kunadokeza pia Mana ya Jangwani yalivyotua duniani kutoka mbinguni. Mana hiyo ni alama ya roho wa wema, uzuri, utajiri, haki, chakula, upendo vilivyoshuka kutoka mbinguni katika Yesu aliye chakula kipya cha roho na mwili. Kadhalika huaa ni alama ya kudumu inayooneshwa na namna njiwa anavyorudi daima kwenye kiota chake. Kwa hiyo Yesu ni makao ya kudumu ya Roho huyo aliye kama hua.

Kisha sauti ikatoka mbinguni “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.” Maneno hayo yanamwelekea kila mmoja wetu Mungu anaposema: “wewe ni mwana wangu mpendwa.” Yesu atayasema maneno hayo katika hotuba yake ya mwisho: “ili ulimwengu wote ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi” (Yoh 17:23), yaani Mungu ananipenda kama alivyompenda Yesu wa Nazareti.

Kwa hiyo, ukimwangalia Yesu utauona uso wa Mungu. Ukiangalia upendo wa Yesu utamwona Mungu, kwani Mungu anakupenda kama ulivyo na hamhukumu mtu mwenye dhambi kwa sababu Mungu ni upendo. Sisi wabatizwa tumeunganika na kushiriki umwana huo wa Mungu katika upendo, tumempokea roho aliyemwingia Yesu. Kwa hiyo hata sisi tumepata mwanga mpya na tumekuwa wana wapendwa wa Mungu. Tunapotamani kuona uso wa Mungu katika Yesu, twaweza kuuona tukimtafakari  mtu yeyote yule aliyeishapata ufunuo huo toka kwa Mungu. Kila mtu anaonesha uso wa kimungu unaongaza, kadhalika katika kila jumuia ya wakristu waliobatizwa kuna uso wa Mungu unaoangaza. Jaribu kuuonesha uso wa Kristu ulio nao kwa kufanya matendo mema ya huruma. Heri kwa Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana na mwanzo mpya wa maisha ya kiroho!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.