2016-01-08 09:45:00

Wakristo wanahamasishwa kuwa ni chemchemi ya furaha kwa jirani zao!


Patriaki Tawadros II wa Kanisa la Kikopitik la Kiorthodox katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa mwaka 2016 anasema Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kuja kukaa kati ya watu wake, lengo ni kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, na hatimaye kumkirimia mwanadamu furaha ya maisha ya uzima wa milele. Hii ndiyo changamoto kubwa kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, katika maisha yao wanajitahidi kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya furaha.

Noeli kwa Makanisa ya Mashariki kwa mwaka huu imeadhimishwa hapo tarehe 7 Januari. Nchini Misri, waamini wameshiriki mkesha wa Noeli na Serikali ilihakikisha kwamba, kunakuwepo na ulinzi na usalama, ili kuwawezesha waamini kusherehekea Noeli kwa amani na utulivu kwa sababu hii ni haki yao kikatiba na kisheria. Katika mkesha wa Noeli kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Marko, mjini Cairo, Rais Abdel Fattah al-Sisi alishiriki na mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, alitoa salam na matashi mema kwa Wakristo na taifa la Misri katika ujumla wake kwa kuadhimisha Siku kuu ya Noeli.

Rais amekemea vikali mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini kwamba, yanahatarisha amani, ustawi na mafungamano ya kijamii. Ameomba radhi kwa Serikali yake kuchelewa kufanya ukarabati mkubwa kwa Makanisa yaliyoharibiwa kutokana na machafuko ya kisiasa nchini Misri kunako mwaka 2013, ambako Makanisa zaidi ya hamsini yaliharibiwa vikali na watu wanaosadikiwa kuwa na misimamo mikali ya kiimani.

Patriaki Tawadros II katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Noeli amekazia umuhimu wa Siku kuu hii inayopyaisha imani, furaha na matumaini ya waamini, huku utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Wachungaji kondeni na Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali wanao mchango mkubwa katika tafakari ya Siku kuu ya Noeli, kwani wao walikuwa ni watu wa kwanza kuguswa na kuonja furaha ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu, wakawa tayari kuwashirikisha wengine kwa njia ya ushuhuda wao.

Lakini ikumbukwe kwamba, furaha ya waamini ni kubwa kwa vile Emmanuel, yaani Mungu ameamua kukaa kati ya watu wake. Kutokana na ukweli huu, Mwenyezi Mungu anakuwa kweli ni kisima cha furaha kwa waja wake, furaha ambayo Wakristo wanapaswa kuishuhudia sanjari na kuwashirikisha majirani zao. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ni mtu mwingine ambaye aliguswa kwa namna ya ajabu na uwepo wa Mungu kati ya watu wake, kiasi cha kuwa ni chemchemi ya furaha na faraja kwa wale wote waliobahatika kukutana na Mtoto Yesu katika hija ya maisha yao.

Furaha ya Bikira Maria inatokana na utakatifu wa maisha kwani ni vigumu sana kuweza kuchuma matunda mazuri kwenye mti mbaya. Kumbe furaha ya taifa lolote lile inabubujika kutoka kwa wananchi ambao ni wema, watakatifu, wenye haki, wakweli na waaminifu. Mamajusi, waliweza kuonesha furaha yao kwa kumpatia Mtoto Yesu zawadi ya dhahabu, uvumba na manemane. Hii ni changamoto kwa waamini kuwa kweli ni chemchemi ya furaha kwa watu wanaowazunguka, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo vya upendo, huruma na faraja.

Wachungaji walionesha furaha yao ya kweli kwa kukesha pamoja na uaminifu wao, mambo msingi katika ujenzi wa jamii inayojikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano. Uaminifu, ukweli na haki ni mambo yanayomfurahisha mwanadamu, furaha ambayo inaweza kumfikia hata Mwenyezi Mungu! Patriaki Tawadros II katika ujumbe wake wa Noeli kwa mwaka 2016 anawataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya furaha na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.