2016-01-08 09:12:00

Lengo ni kudumisha mshikamano wa upendo kwa ajili ya mafao ya wengi!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Januari 2016 anatarajiwa kutembelea Hekalu kuu la waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma, kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha umoja, udugu, upendo, mshikamano na majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Hili litakuwa ni tukio la kihistoria katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwa kuwa na uelewa sahihi wa dini na mchango wake katika maisha ya wananchi.

Mwenyezi Mungu ni asili na chemchemi ya wema, upendo na utakatifu wa maisha, kumbe waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kuwa na ufahamu bora zaidi wa mafundisho ya dini zao, tayari kukataa kishawishi cha kutaka kutumbukizwa kwenye vita, machafuko, nyanyaso na dhuluma na watu wachache wenye misimamo mikali ya kidini. Hivi ndivyo anavyosema Riccardo Di Segni, Rabbi mkuu wa waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma.

Rabbi Di Segni anaendelea kufafanua kwamba, kuna tofauti kubwa kati ya hija ya kwanza iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II Hekaluni hapo, takribani miaka thelathini iliyopita kwani haya yalikuwa ni mapinduzi makubwa ya mahusiano kati ya Wayahudi na Wakristo. Papa mstaafu Benedikto XVI akaendelea kuimarisha mahusiano haya kwa kutembelea Hekaluni hapo. Riccardo Si Segni anasema, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alikuwa na uhusiano wa pekee na Jumuiya ya Kiyahudi hususan kutokana na mchango wake katika masuala ya kitaalimungu yaliyonesha hekima na utaratibu wa maisha.

Jumuiya ya Kiyahudi mjini Roma inajiandaa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, mtu wa watu ambaye maisha yake kwa kiasi kikubwa yanajikita katika shughuli za kichungaji. Papa Francisko anataka kukutana, kuzungumza na kusalimiana na watu, ili kuwashirikisha ile furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yake. Wayahudi wengi wanatamani kukutana na kushikana mkono na Baba Mtakatifu, ili kusonga mbele katika mchakato wa kudumisha majadiliano ya kidini katika umoja, udugu na urafiki, mambo ambayo ni sehemu ya maisha ya waamini.

Rabbi Di Segni anasema, Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Jumuiya ya Kiyahudi wakati huu Kanisa Katoliki linaendelea kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; miaka ishirini ya majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na mkesha wa Juma la kuombea Umoja wa Wakristo. Matukio yote haya yanaifanya hija ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Hekalu kuu la waamini wa dini ya Kiyahudi mjini Roma kuwa na alama ya neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Jubilei inapata chimbuko na maana yake kutoka katika Maandiko Matakatifu.

Rabbi Riccardo Di Segni anasema, tukio la Baba Mtakatifu Francisko kuwatembelea Wayahudi ni kuonesha kwamba, hapa kuna dini mbili tofauti, lakini waamini wa dini hizi wanaweza kuishi kwa amani, upendo, umoja na udugu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Huu ndio ujumbe unaopaswa kubaki ukiwa umepigwa chapa katika akili na mioyo ya waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.