2016-01-07 17:16:00

Yaliyojiri wakati wa ziara ya Waziri mkuu Majaliwa mkoani Ruvuma!


Waziri mkuu wa Tanzania amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea kiwanda cha Tumbaku mkoani Ruvuma pamoja na kuwasimamisha kazi viongozi wa Chama cha Ushirika cha SONAMCU. Waziri mkuu amekagua Jengo la Makao makuu ya Wilaya ya Halmashauri ya Songea pamoja na kufungua Twi la Benki ya Posta Songea. Amekagua maghala ya wakala wa hifadhi ya taifa ya chakula Kanda ya Songea. Kwa ufafanuzi zaidi, unaweza kuendelea “kujinafsi” mwenyewe!

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha kusindika tumbaku cha mkoani Ruvuma na kuwasimamisha kazi viongozi wa Chama Kikuu Cha Ushirika cha SONAMCU. Akizungumza siku ya Jumanne, Januari 5, 2016, katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu Ndogo ya Songea, wakati alipokutana na wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Namtumbo, Wananchama wa Vyama Vya Ushirika vya Mkoa wa Ruvuma, viongozi wa Mkoa pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini.

Waziri Mkuu amesema, Serikali ina dhamira ya kufufua kiwanda cha kusindika tumbaku cha SONAMCU, na lengo la kutembelea kiwanda hicho ni katika utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli la kufufua viwanda nchini. Waziri Mkuu Majaliwa, ametembelea maeneno mbalimbali ya kiwanda hicho na kukagua mitambo iliyokua ikitumika kusindika tumbaku, kabla kiwanda hicho kuzimwa miaka kadhaa iliyopita baada ya kukosa malighafi za kuendelea na uzalishaji.

Pia, amemtaka Afisa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bibi. Stela Lugongo kuandaa na kuwasilisha kwake mkakati wa kufufua kiwanda hicho cha kusindika tumbaku, na baadae kuwasimamisha kazi viongozi wote wa Chama Kikuu cha Ushirika cha SONAMCU waliohusika na tuhuma hizo na kutaka wafikishwe Mahakamani. “Serikali imeazimia kufufua viwanda, hasa vile ambavyo havina wawekezaji vimebaki vyenyewe, Tunahitaji kujua namna ya kuvifufua”. Alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa pia, amesikiliza na kujibu kero mbalimbali za wakulima wa tumbaku wa Mkoa huo, ambao walilalamikia mfumo wa Vyama vya Ushirika na namna ambavyo vyama hivi vimekua vikiwaibia fedha zao hadi kushindwa kuendelea kulima zao la tumbaku na kukosa masoko ya mazao yao.

Aidha, Waziri Mkuu amewasihi wakulima kuwa watulivu na kusubiri maamuzi ya Mahakama baada ya kuwa viongozi wa Chama cha Ushirika SONAMCU ambao wamehusika na wizi wa fedha za wakulima kiashi cha Shilingi milioni 800 kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi 2014 tayari wamefikishwa Mahakamani na uchunguzi unaendelea. Pia, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu kukutana na wakulima hao ili kupatia ufumbuzi matatizo yao.

Aidha, ametoa wito kwa wakulima kuendelea kulima zao la tumbaku kwa kuwa linaongeza pato la mtu mmoja mmoja, linasaidia kuchangia pato la Mkoa na kukua kwa uchumi wa nchi. Amewashauri wakulima kuunda na kuviendesha Vyama Vya Ushirika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wialaya ya Songea lilipo katika kijiji cha Lundusi, Wilaya ya Peramiho mkoani Ruvuma.  Alipowasili  katika eneo hilo alikutana na viongozi wa jadi ambapo Mzee Daniel Gama alimkabidhi ngao na silaha ikiwa ni ishara ya kumkaribisha kijijini hapo, pia alipata fursa ya kutazama ngoma ya mila ya kabila la Wangoni.

Mara baada ya kukagua jengo hilo la ghorofa,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lundusi Bwana Rajabu Mtiula amesema jengo hilo lenye ofisi 50, vyoo 4, ukumbi mkubwa 1 na kumbi ndogo 2, ambapo mradi huo umetekelezwa kwa fedha za mfuko wa Mradi wa Maendeleo na Serikali. Hadi sasa Serikali imetoa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 200 na utekelezaji wake umekamika kwa 85%, hivyo wanatarajia kuanza kutumia jengo hilo mwezi Februari, 2016.

Akizungumza siku ya Jumatatu, Januari 4, 2016 na wananchi wa kijiji cha Lundusi, Waziri Mkuu, amewapongeza wananchi wa Lundusi kwa hatua hiyo ya maendeleo na kusema kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono ujenzi wa jengo hilo. Waziri Mkuu Majaliwa, ametaka kuwepo na mikakati ya uboreshaji wa eneo hilo kwa kusogeza huduma karibu ili kuvutia watu zaidi katika eneo hilo.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Uratibu, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama ametoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli na Waziri Mkuu kwa kuchaguliwa na kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano. Pia, ameishukuru Serikali kwa kusaidia kujenga jengo hilo, na pia ameeleza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo ikiwemo wakulima kutofaidika kwa bei ya soko ya kuuza mahindi, kutokuwepo na umeme na maji.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza Waziri Jenista kufuatilia kero hizo kwa Wizara husika na baadae kuleta mrejesho kwa wananchi.  Waziri Mkuu Majaliwa anaendelea na ziara mkoani Ruvuma, Siku ya jumanne Januari 5, 2016 atatembelea na kukagua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kuongea na Watumishi wa hospitali hiyo na baadae ataongea na Watumishi wa Umma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefungua tawi la Benki ya Posta iliyopo mjini Songea, wakati akiwa katika ziara mkoni Ruvuma inayotarajiwa kumalizika jumatano ijayo. Akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa Benki ya Posta pamoja na wateja waliohudhuria ufunguzi wa tawi hilo uliofanyika nje ya benki hiyo hapo jana, Waziri Mkuu amesema amefarijika kuona benki hiyo iliyokua imekumbwa na matatizo sasa imezaliwa upya na kumpongeza Mkurugenzi wa Benki ya Posta nchini Bwana. Sabasaba Mushindi kwa jitihada zake za kufufua benki hiyo.

Amesema, Benki hiyo inalenga wananchi wenye vipato vya chini, SACOSS, Vyama Vya Ushirika na wafanyabiashara wadogo wadogo , nakusisitiza kuwa wafanyabishahara na wananchi wa Ruvuma wanaweza kukopa ili kukuza mitaji yao lakini waweze kurudisha mikopo hiyo ili iwanufaishe na wengine.

Waziri Mkuu Majaliwa, pia amefurahishwa na huduma ya mikopo kwa wasataafu inayotolewa na benki hiyo, ambapo amesema amefarijika kuona wazee nao wana nafasi ya kukopa kupitia benki ya posta. Pia, ametumia fursa hiyo kutoa wito wa kuwataka watanzania kuacha tabia ya kutembea na fedha nyingi mifukoni kwani hukaribisha wizi na kusababisha matumizi yasiyo na mpangilio. “Watanzania tubadilike , ni muhimu sasa watanzania kubadilika tuhifadhi fedha zetu Benki” alisema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta nchini Bwana. Sabasaba Mushindi amempongeza Waziri Mkuu na Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kuchaguliwa na wananchi na namna ambavyo wameendelea kuingoza Serikali chini ya kauli mbiu ya HAPA KAZI TU.

Bwana. Mushindi amesema benki ya Posta ilianzishwa miaka 90 iliyopita ikiwa chini ya utawala wa kikoloni, ina lengo la kuchochea utamaduni wa kujiwekea akiba kwa watanzania, takwimu zikionesha watanzania wako nyuma katika kuweka akiba. Chini ya 10% ya mapato ndio yanawekwa kama akiba, na 14% ya watanzania wanaohifadhi fedha benki, na 3% tu ya watanzania wana sifa na uwezo wa kukopa benki.

Aidha, amesema baada ya kukabiliana na changamoto mbalimbali hivi sasa benki ya Posta inaendelea kuimarika ambapo wamekua wakipata faida na baada ya mahesabu kukamilika wanatarajia kupata hadi kiasi cha bilioni 12 kwa mwaka 2015.  “Hadi sasa 70% ya matawi ya benki yamefanyiwa ukarabati, kumekuwepo na huduma kama PPT popote, akaunti ya michezo (Sports account) ambayo imesaidia vilabu mbalimbali kama Mbeya City na Stand United ya Shinyanga, pia benki imetoa kiasi cha shilingi milioni 150 kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii ” alisema Bwana. Mushindi

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea, wakati akiendelea na ziara yake mkoani Ruvuma. Akizungumza na wafanyakazi wa Wakala hiyo, wadau wa kilimo pamoja na wananchi Jumatatu, Januari 4, 2016 nje ya majengo ya Wakala mara baada ya kukagua mahindi yaliyohifadhiwa katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , mkoani Ruvuma amesema kufuatia taarifa ya kuwepo na baadhi ya maeneo yenye njaa nchini, Serikali imetoa tamko kuwa hakuna mtanzania atayakekufa kwa njaa.

Ambapo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa imeweka mikakati ya kukabiliana na tatizo la njaa kwa kutoa msaada wa chakula katika maeneo yanayokabiliwa na njaa.  “Ni wajibu wangu kuhakikisha nasimamia vizuri hili, nimeona hali ya uhifadhi wa chakula, tunayo mahindi ya kutosha lakini hakuna sehemu ya kuhifadhi chakula”amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa ameendelea kwa kusema uwezo wa maghala hayo yaliyopo chini ya Wakala Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea yana uwezo wa kuhifadhi tani 29 pekee na Songea inauwezo wa kuzalisha zaidi tani 70 hadi 80. Pia, ameagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea , kuanzia mwaka huu kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa pamoja Wakuu wa Wilaya kuanzisha vituo vya kununulia mahindi na kuhakikisha magunia yanawafikia wakulima katika vituo hivyo ambapo wataweza kuhifadhi mahindi na kuuza kwa bei ya kwenye soko.

Waziri Mkuu pia, ameitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songea ,kutumia teknolojia ya kisasa ya uhifadhi wa chakula, kuandaa utaratibu maalum utakaozuia msongamano wa malori yanayosubiri kupata huduma ya kununua mahindi nje ya majengo ya Wakala na kukamilisha miradi itakayosaidia Wakala kuwa na fedha za kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake, Meneja Hifadhi wa Chakula kanda ya Songea, Bwana. Morgan Mwaipaya amesema kati ya maghala 33 ya kuhifadhi mahindi nchi nzima, Songea ina maghala 6 kati ya hayo. Hivyo, Wakala imeweka vipaumbele vyake ambavyo ni pamoja na kutoa chakula cha msaada kwa maeneo yenye matatizo ya njaa, kuongeza upatikanaji wa mahindi ili kuzuia kupanda kwa bei ya chakula mwaka 2015 – 2016, Wakala kununua na kuhifadhi mahindi katika maeneo yaliyozalisha zaidi na kuzingatia sehemu ya sehemu ya akiba ya chakula na kuuza kwa wakulima, mawakala pamoja na Wakala wa Chakula Duniani (World food program).

Amesema Wakala imeandaa mikakati ya mbalimbali ikiwemo kuongeza uwezo wa tani 24600 hadi tani 45000 kwa mwaka 2014- 2017, kuboresha mfumo wa utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya stahili ya TEHAMA na kutumia fursa za mikopo kutoka Taasisi mbalimbali za kifedha ili kuendesha shughuli za uwezeshaji I kiwemo kuelimisha taratibu za ununuzi kwa mawakala.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Songea, Mheshimiwa Leonidas Gama amesema wakulima wachache wamekua wakiuza mahindi yao kwa bei ya soko, wengi wao wamekua wakiuza mahindi kwa mawakala kwa bei ya shilingi 150 hadi 200 kwa kilo na wakala wakiuza kwa shilingi 500 kwa Serikali. Ambapo amemuomba Waziri Mkuu kutatua tatizo la soko la mahindi kwa wakulima. Hata hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima kuendelea kuzalisha mahindi akiahidi Serikali kununua mahindi hayo kwa bei ya soko ambayo itamnufaisha mkulima.

Imetolewa na Ofisi ya Waziri mkuu.








All the contents on this site are copyrighted ©.