2016-01-07 16:31:00

Kampeni ya kuhamasisha mchakato wa amani Syria yazinduliwa rasmi!


Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, mwanzoni mwa Mwaka 2016 limezindua kampeni ya kimataifa inayolenga kuwahamasisha wadau kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kusimama kidete na kuhakikisha kwamba, haki, amani na maridhiano vinarejeshwa tena nchini Syria, ambako hadi sasa watu wanaendelea kukabiliana na utamaduni wa kifo unaojikita katika nyanyaso, dhuluma na mauaji kwa misingi ya udini. Kwa muda wa miaka mitano, Syria imekuwa ikitawaliwa kwa mtutu wa bunduki, hali ambayo imepelekea uwepo wa mpasuko wa kijamii katika Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Caritas Internationalis inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha tena mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili haki, amani na maridhiano yaweze kutawala tena katika mioyo na akili za watu, huku wakiendelea kujikita katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa. Majadiliano haya yanapaswa kuzihusisha pande zote zinazohusika, ili kweli amani iweze kupatikana. Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inaweza kuibuliwa na wahusika wenyewe na wala si kwa kupandikizwa kutoka nje ya Syria. Hii itakuwa ni amani inayoonekana kwenye makaratasi, lakini huko mitaani watu wataendelea kupambana na mtutu wa bunduki!

Wananchi wa Syria wanataka haki, amani na maridhiano na wala si mkate wala fedha kwani wakiwa na amani, usalama na utulivu wataweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na huduma. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kutambua kwamba, mgogoro wa Syria hauwezi kusuluhishwa kwa njia ya mtutu wa bunduki, bali kwa njia ya majadiliano ya kisiasa, vinginevyo, kila upande utaendelea kutunisha misuli na wanaoathirika na wananchi wasiokuwa na hatia.

Jumuiya ya Kimataifa iunge mkono majadiliano ya kisiasa, ili hatimaye kuunda Serikali ya mpito itakayohakikisha ujenzi wa umoja wa kitaifa pamoja na kudhibiti biashara haramu ya silaha inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, huku watu wachache wenye uchu wa fedha na utajiri wa haraka haraka wakiendelea kuchuma fedha inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia! Wananchi wanatamani kuona haki, amani na usalama vikirejea tena nchini Syria. Watu wanaamini kwamba, inawezekana Syria kupata amani tena, ikiwa kama kila upande utaonesha utashi wa kisiasa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Vita ambayo imedumu kwa muda wa miaka mitano imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Leo Syria ambayo ilikuwa na vielelezo vingi vya kitamaduni na maendeleo makubwa kw awatu wake, imegeuka kuwa ni magofu na uwanja wa fujo na mauaji. Rasilimali watu imepotea na kutoweka; viwanda na sehemu za huduma za kijamii zimeharibiwa na vita na wananchi kwa sasa wamekuwa ni wakimbizi na wahamiaji; watu ambao hatima ya maisha yao iko wakati mwingine mikononi mwa wafanyabiashara ya binadamu na viungo vyake.

Wananchi wa Syria wanatembea na kifo miguuni pao, leo hii hata wakizama na kufa maji, si habari tena inayowagusa walimwengu! Watu wamekuwa baridi kiasi hata cha kushindwa kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wanachi wa Syria. Watu wamegeuka kuwa maskini wa hali na kipato. Lakini bado wananchi wanataka kuona Syria ikiandika ukurasa mpya wa maisha yake inayojikita katika misingi ya haki, amani, maridhiano na usalama. Wananchi wamechoka na vita wanataka amani, usalama na utulivu inasema  Caritas Internationalis.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.