2016-01-07 08:26:00

Chuo kikuu cha Garissa, Kenya chafunguliwa tena kwa kishindo!


Serikali ya Kenya imedhamiria kuhakikisha kwamba, inaendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi kwa kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria, ili kutoa mwanya kwa mchakato wa maendeleo kwa njia ya elimu kushika kasi! Serikali ya Kenya baada ya kufunga Chuo kikuu cha Garissa kutokana na mauaji ya wanafunzi 147 yaliyofanywa na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab kutoka Somalia, kimefunguliwa tena kwa kishindo kikuu, ili kuwahakikishia wananchi wa Kenya kwamba, Serikali inapania kuwalinda raia na mali zao.

Itakumbukwa kwamba mauaji ya kutisha huko Garissa yalifanyika hapo tarehe 2 Aprili 2015. Mashambulizi haya yalidumu kwa takribani masaa sita, wanajeshi wa kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab walipowavamia wanafunzi wakiwa bado usingizini na kusababisha mauaji ya kinyama na wengine wengi kupata majeraha ya kudumu, wale waliofanikiwa walikimbia ili kusalimisha maisha yao. Wakati wa uzinduzi wa Chuo kikuu cha Garissa baadhi ya wanafunzi walikuwa bado wanaonesha machungu waliyokumbana nayo wakati wa mauaji yale.

Taarifa inaonesha kwamba, kwa sasa walioanza kazi ni wafanyakazi, walimu na wanafunzi wanatarajiwa kuanza kuingia tarehe 11 Januari 2016. Hili ni tukio la kihistoria anasema Bwana Ahmed Osman Warfa, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Garissa anayekazia kwamba, hawataruhusu watu wachache wawapokonye wananchi hazina hii muhimu sana katika maendeleo yao. Mikakati ya ulinzi na usalama imeendelea kuimarishwa Chuoni hapo kwa kuweka pia Kituo kidogo cha Polisi kinachohudumiwa na Askari 25.

Wanafunzi 650 waliosalimika jaribio la mauaji wakati ule, ambao kwa sasa wanapatiwa hifadhi kwenye Chuo kikuu cha Eldoret, hawatalazimika kurejea tena kwenye Chuo kikuu cha Garissa. Ujumbe wa upendo, haki, amani na mshikamano umeoneshwa na wananchi wengi wa Kenya pamoja na wapenda amani kwa kutambua kwamba, elimu ni silaha makini katika kupambana na vitendo vya kigaidi unaokumbatiwa na utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.