2016-01-06 15:35:00

Maandamano ya "Viva Befana" yawakuna wengi mjini Vatican


Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2016 mjini Vatican yalipambwa kwa maandamano makubwa ya mahujaji waliokuwa wamevalia nguo za kitamaduni, wakiongozwa na bendi za muziki na mashangilio mbali mbali, walipita kwa mbwembwe na maringo kwenye viunga vya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hadi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu, ili kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa Sala ya Malaika wa Bwana baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Maandamano haya ambayo yalianzishwa kunako mwaka 1985, maarufu kama “Viva la Befana” kwa mwaka huu yanatimiza miaka thelathini na moja wa uwepo wake, tukio ambalo limekuwa na mvuto mkubwa kwa wasanii wenyewe na mahujaji wanaomiminika kila mwaka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana.

Lengo ni kutaka kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho zinazofumbatwa katika maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, yaani Kristo Mwanga wa Mataifa anapojidhihirisha kwa watu wa mataifa mbali mbali duniani, wakiwakilishwa na Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali.

Hawa ni watu kutoka katika kila kabila, lugha na jamaa, wanaotaka kumwona Mtoto Yesu ili kumtolea zawadi na shukrani kwa wema na ukarimu wake, hasa kwa mwaka huu, Kanisa linapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wanahamasishwa kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao: kiroho na kimwili. Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, wawakilishi wa Mamajusi watatu walikwenda kutoa zawadi zao kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.