2016-01-06 14:41:00

Itafuteni nyota angavu ili iwaongoze katika maisha yenu!


Nabii Isaya anawambia Waisraeli “Ondoka Ee Yerusalemu, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja na utukufu wa Bwana umekuzukia. Huu ni mwaliko kwa waamini kutoka huko walikojificha na katika ubinafsi wao, ili wawe tayari kutambua mwanga unaoangazia maisha yao na kwamba, mwanga na utukufu wa Mungu utawazukia. Kanisa ni mwanga unaongaza utukufu wa Kristo unaojikita katika haki, kiasi kwamba, Kanisa linaishi na kudumu kutokana na mwanga wa Kristo Yesu anayeishi ndani mwake.

Kristo ni mwanga angavu unaofukuza giza, kumbe, Kanisa linapaswa kumwambata Kristo, ili liweze kuwa ni nuru ya mapito ya watu wa mataifa. Kutokana na mwelekeo huu, Mababa wa Kanisa wanalitambua Kanisa kuwa ni Fumbo la Mwanga! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sherehe ya Tokeo la Bwana ambayo inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, familia ya Mungu inahitaji nuru hii ili iweze kuangazia wito iliyopokea wa kumtangaza na kumshuhudia Yesu Kristo. Kanisa linatambua kwamba, umissionari ni sehemu ya dhamana na vinasaba vya maisha na utume wake, vinavyopaswa kupata mwanga wa Mungu. Kuna mamillioni ya watu wenye kiu ya kutaka kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa masikioni mwao, kwani wanataka kumwambata Kristo, wanataka kuona uso wa Baba.

Mamajusi wanaosimuliwa na Mwinjili Mathayo ni mashuhuda hai mbegu ya ukweli iliyopandikizwa sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, ni Mwenyezi Mungu, Muumba wa vyote anayewaalika kumfahamu Mungu kuwa ni Baba na Mwaminifu. Mamajusi ni wawakilishi wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaopokelewa nyumbani kwa Mungu. Mbele ya Yesu Kristo hakuna tena utengano wa kabila, rangi, lugha na tamaduni: mbele ya Mtoto Yesu, binadamu wote wanaunganishwa katika umoja.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Kanisa lina dhamana ya kuhakikisha kwamba, linaonesha wazi wazi utashi wa Mungu unaofumbatwa katika maisha ya kila mwanadamu. Hata leo hii kama ilivyokuwa wakati wa Mamajusi bado kuna watu wenye wasi wasi na mashaka mioyoni, wanaoendelea kujiuliza maswali mengi, lakini pasi na majibu muafaka. Hawa pia ni watu wanaotafuta Nyota angavu itakayowaelekeza njia ya kwenda Bethlehemu.

Baba Mtakatifu anasema, kuna nyota nyingi mbinguni, lakini, Mamajusi waliamua kufuata nyota moja tu iliyokuwa inaangaza zaidi. Ni watu waliokuwa wamejifunza kwa kina na mapana kitabu cha mbinguni ili kupata majibu ya maswali yao msingi, hatimaye, wakafanikiwa kuona mwanga wa nyota ambayo ilileta mabadiliko makubwa katika maisha yao. Wakaacha mambo yao ya kila siku na kuanza kushika njia ili kuitafuta nyota hii, kwa kusikiliza dhamiri nyofu iliyokuwa ndani mwao, ikiwasukuma kufuata ule mwanga; ikawaongoza hadi walipofika na kumwona Mfalme wa wa Wayahudi, akiwa nyumbani Bethlehemu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, yote haya ni mafundisho makini yanayopaswa kuzingatiwa na waamini kwa kujiuliza swali msingi “ Yuko wapi Yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake Mashariki, nasi tumekuja kumsujudia”. Waamini wanaoishi nyakati kama hizi wanahamasishwa kuhakikisha kwamba,  wanayatafuta mapenzi ya Mungu; wanajihimu kwenda Bethlehemu ili kumwona Mtoto na Mama yake.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufuata nuru ya nyota wanayooneshwa na Mwenyezi Mungu; Nuru inayoangaza uso wa Kristo, mwingi wa huruma na uaminifu. Baada ya kufika mbele ya Mtoto Yesu, wamwabudu kwa moyo wote na kumpatia zawadi zao: yaani: uhuru, akili na upendo. Waamini watambue kwamba hekima ya kweli inajificha katika uso wa Mtoto Yesu. Katika hali ya kawaida kabisa, Bethlehemu unakuwa ni muhtasari wa maisha ya Kanisa. Hapa ni mahali ambapo ile nuru angavu yenye mvuto inapojionesha na kuongoza watu katika njia ya amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.