2016-01-05 11:33:00

Wakristo Nchi Takatifu wanataka haki na amani na wala si upendeleo!


Maaskofu Waratibu wa Nchi Takatifu ni kikundi kinachoundwa na Maaskofu kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya, Canada na Afrika ya Kusini, ambacho kiko mstari wa mbele katika kusaidia kufadhili maisha na utume wa Kanisa katika Nchi Takatifu. Maaskofu hawa kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 17 Januari 2016 wanatembelea sehemu mbali mbali za Nchi Takatifu ili kujionea wenyewe hali halisi, tayari kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia.

Wakiwa katika Nchi Takatifu, Maaskofu hawa wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, lakini kwa namna ya pekee, katika Parokia ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Fumbo la Umwilisho. Wakiwa Parokiani hapo, Maaskofu watakutana na kuzungumza na waamini pamoja na kutembelea miradi mbali mbali inayogharimiwa na Kikundi hiki cha Maaskofu kwa ajili ya waathirika wa machafuko ya kisiasa ya mwaka 2014.

Katika kipindi cha miaka mitatu, Maaskofu hawa wamekuwa wakitembelea Ukanda wa Ghaza, eneo ambalo idadi ya Wakristo inaendelea kupungua kila mwaka kutokana na kinzani za kisiasa pamoja na ujenzi wa ukuta unaowatenganisha watu. Maaskofu pia watapata nafasi ya kutembele nchini Yordan kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 14 Januari, ili kuwashirikisha wahamiaji na wakimbizi ujumbe wa upendo na mshikamano, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Huu ni mwaliko wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni wakimbizi wanaotoka Syria na Iraq ambako machafuko ya vita yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kikundi hiki cha Maaskofu kinapania kulisaidia Kanisa mahalia Nchi Takatifu ili liweze kutekeleza dhamana na utume wake kwa njia hali na mali, pamoja na kuonesha Jumuiya ya Kimataifa kile kinachotendeka katika maeneo haya. Waamini wanaoishi kwenye Nchi Takatifu wanataka haki na amani na wala si upendeleo, ili waendelee kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mshikamano huu wa upendo kutoka kwa Maaskofu ulianzishwa kunako mwaka 1998 na unatekelezwa kila mwaka ifikapo mwezi Januari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.