2016-01-05 15:06:00

Sura ya huruma ya Mungu kwa maskini na wanyonge mjini Jakarta


Kipindi cha maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, Jimbo kuu la Jakarta, Indonesia, kimekuwa ni wakati muafaka wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya huruma ya Mungu. Imekuwa ni nafasi pia ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, ili kuendeleza mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kwa kutambua kwamba, tofauti zao za kiimani si sababu msingi ya kuwagawa bali ni utajiri unaopaswa kuheshimiwa na kuendelezwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wote.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma, wakati wa Siku kuu ya Noeli, iliandaa chakula kwa maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sehemu mbali mbali za Indonesia, ili kuonesha mshikamano wa huruma na mapendo. Kwa njia hii waamini wa dini mbali mbali waliweza kuungana na kusherehekea kwa pamoja zawadi ya maisha kwa kuzaliwa kwa Kristo Mkombozi wa dunia, Mfalme wa amani.

Huduma ya mapendo, imekuwa ni kikolezo muhimu sana kwa waamini wa dini mbali mbali kushirikiana kwa dhati nchini Indonesia ambako takwimu zinaonesha kwamba, waamini wa dini ya Kiislam ni asilimia 87% ya idadi yote ya wananchi wa Indonesia. Hapa wananchi wanahamasishwa kujenga umoja katika utofauti kama wanavyoungama katika Katiba ya nchi yao. Sheria hii mama inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, vinginevyo, Katiba itakuwepo lakini bado kinzani na migawanyiko kwa misingi ya kidini itaendelea kutawala na kuwasambaratisha watu.

Kwa namna ya pekee, Noeli ya Mwaka uliopita, iliangukia siku ya Ijumaa, kumbe waamini wa dini ya Kiislam walipotoka katika swala ya Ijumaa, wakaungana na wenzao kwa chakula cha mchana. Askofu mkuu Ignatius Suhario Hardjoatmodjo wa Jimbo kuu la Jakarta anasema, hili limekuwa ni tukio linaonesha huruma ya Mungu kwa waja wake, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa watu kuoneshana upendo na mshikamano, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Noeli imekuwa ni Siku kuu ya huruma ya Mungu kwa watu wote, matendo makuu ya Mungu. Vyama mbali mbali vya kitume vimeonesha ukarimu pamoja na kuchangia ustawi na maendeleo ya wengi, hali ambayo inaendelea kukata mzizi wa fitina, woga, wasi wasi na hali ya waamini wa dini hizi mbili kutoaminiana. Lakini, waamini wanapaswa kushinda ubaya kwa kutenda mema.

Kanisa Katoliki nchini Indonesia linataka kuacha chapa ya changamoto ya huruma ya Mungu iliyoachwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka hamsini iliyopita! Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu Francisko, mambo mazuri si habari inayochangamkiwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.