2016-01-05 08:34:00

Papa atembelea Madhabahu ya Greccio, Pango la kwanza la Mtoto Yesu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 4 Januari 2016 amefanya ziara binafsi kwenye Madhabahu ya Wafranciskani yaliyoko huko Greccio, mahali ambapo Mtakatifu Francisko wa Assisi alianzisha utamaduni wa kutengeneza Pango la Mtoto Yesu. Baba Mtakatifu amepata chakula cha mchana na Askofu Domenico Pompili wa Jimbo Katoliki Rieti, Italia na baadaye kutembelea Madhabahu ya Greccio na kusali kwa kitambo kidogo. Papa amepata pia nafasi ya kukutana na Wafranciskani wanaoishi katika eneo hili pamoja na kuzungumza na kundi la vijana kutoka sehemu mbali mbali za Italia ambao wamekusanyika Jimboni Rieti ili kutafakari kuhusu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Sifa kwako, juu ya utunzaji wa nyumba ya wote, Laudato si!

Baba Mtakatifu akizungumza na vijana hawa amewataka kujenga na kukuza ndani mwao fadhila ya unyenyekevu itakayowasaidia kupambana na changamoto mbali mbali za maisha. Imani iwe ni dira katika maisha yao. Baba Mtakatifu amesali kwa kitambo pamoja na Wafranciskani wanaoishi na kufanya kazi katika Madhabahu ya Greccio, mahali ambapo kunako mwaka 1223, Mtakatifu Francisko alianzisha Pango la Mtoto Yesu, akiwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kuhusu Fumbo la Umwilisho.

Askofu Domenico Pampili anasema, kwake binafsi na kwa familia ya Mungu Jimboni Rieti imekuwa ni fursa ya kushangaa matendo makuu ya Mungu. Baba Mtakatifu amefurahishwa na utunzaji bora wa mazingira unaoendelezwa sehemu hizi. Baba Mtakatifu alikuwa na hamu ya kutembelea eneo ambalo Mtakatifu Francisko alianzisha kwa mara ya kwanza kutengeneza Pango la Mtoto Yesu, akitumia watu halisi, lakini leo hii mambo yamebadilika, kwenye Pango la Mtoto Yesu waamini wanatumia  sanamu.

Baba Mtakatifu amefanya ziara hii binafsi, ili kujipatia nafasi ya kusali na kumshukuru Mungu kwa mema mengi anayoendelea kulijalia Kanisa. Kabla ya kuondoka Madhabahuni hapo ameandika tafakari fupi kwenye Kitabu cha wageni kwa kumshukuru Mungu kwa kumkirimia furaha hii, anamwomba, ili aweze kulibariki Kanisa, Askofu wa Rieti, Watawa na Waamini walei. Mwenyezi Mungu awasaidie waamini kugundua ile Nyota angavu, tayari kujitosa kimasomamo kwenda kumtafuta, ili hatimaye kumwona Mtoto Yesu. 

Hii ni tafakari ambayo inawaandaa waamini kuadhimisha Siku kuu ya Tokeo la Bwana, maarufu kama Epifania. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Siku kuu hii kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:00 za asubuhi kwa saa za Ulaya

Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1983, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea na kusali katika madhabahu haya. Wafranciskani wanaoishi na kuhudumia Mabadhahu haya wamepigwa na bumbuwazi, kiasi hata cha kukosa maneno, kwa kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye ziara yake hapo Greccio ilikuwa inafahamika na watu wachache kabisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.