2016-01-05 10:32:00

Lango la Huruma ya Mungu Madhabahu ya "Divino Amore" Roma!


Katika maadhimisho ya Siku kuuya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2016, Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa “Divino Amore” iliyopo Jimbo kuu la Roma sanjari na kufungua Lango la huruma ya Mungu, kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hapa mwaliko ni waamini kuuvua utu wao wa kale na kuanza kuambata huruma ya Mungu inayojikita katika toba na wongofu wa ndani pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Kardinali Vallini, baada ya kuhitimisha Liturujia la kufungua Lango Takatifu, atakuwa wa kwanza kupitia Lango hili akiwa amebeba Injiili, mwaliko kwa waamini kufuata mwanga wa Injili katika maisha yao, tayari kumshuhudia Kristo, Mwanga wa Mataifa kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo yao adili; daima wakiwa tayari kuyatakatifuza malimwengu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kardinali Vallini ataongoza maandamano kuelekea kwenye Madhabahu Mapya na hapo ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana. Madhabahu haya ni sehemu muhimu sana kwa hija ya waamini wa Jimbo kuu la Roma na majimbo mengine ya jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.