2016-01-04 08:03:00

Zaidi ya watu 11, 000 wameuwawa kikatili na Boko Haram kwa mwaka 2015


Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kinachoendesha mashambulizi ya kujitoa mhanga huko Kaskazini mwa Nigeria, bado ni tishio kubwa kwa usalama na maisha ya wananchi wa Nigeria na nchi jirani za Chad, Niger na Cameroon. Hiki ni kikundi ambacho kinahusika na utekaji nyara wa wanafunzi 200 ambao hadi leo hii hawajulikani mahali walipo, licha ya juhudi za Serikali za kuwatafuta ili kuweza kuwarejesha tena kwa wazazi wao.

Takwimu zilizotolea hivi karibuni na Baraza na Mahusiano ya Kimataifa nchini Nigeria zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015, Boko Haram imesababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia elfu kumi na moja ndani na nje ya Nigeria. Hivi karibuni majeshi ya ulinzi na usalama kutoka Nigeria, Chad, Niger na Cameroon yaliunganisha nguvu ili kupambana na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, lakini hadi sasa bado hawajafanikiwa kukisambaratisha na inaonekana kana kwamba, kinaendelea kupata nguvu na kusonga mbele, huku kikisababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Wakati Boko Haram inaendelea kusumbua ndani na nje ya Nigeria, kwa upande mwingine, Afrika Mashariki, inapambana na kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab, kutoka Somalia. Kikundi hiki kimekuwa ni chanzo cha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia ndani na nje ya Somalia hata wakati mwingine kwa misingi ya udini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.