2016-01-04 07:29:00

Wananchi wanataka mabadiliko ili kuandika upya historia ya nchi yao!


Askofu mkuu Franco Coppola, Balozi wa Vatican nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo sanjari na uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni ni matukio muhimu sana katika maisha ya wananchi wa Afrika ya Kati wanaotaka kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha na maendeleo yao kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, umoja, upatanisho na msamaha, tayari kujikita katika ustawi na maendeleo ya wengi.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu lilikuwa ni tukio la pekee kabisa ambalo liliwakutanisha wanasiasa, waamini wa dini mbali mbali na wananchi katika ujumla wao, ili kuangaliana uso kwa uso bila kuweka miwani ya jua. Wananchi wakaanza kutambuana na kufahamiana, kiasi hata cha kuweka kando silaha ili kuanza mchakato wa demokrasia inayojikita katika misingi ya ukweli na uwazi.

Wananchi wengi wamejitokeza katika kupiga kura pasi na woga wala wasi wasi wa kushambuliwa na kwamba, yote yametendeka katika hali ya amani na utulivu, kielelezo kwamba, wananchi wamechoka na vita, wanataka kuanza ukurasa mpya wa maisha yao. Hija ya Baba Mtakatifu imeacha alama ya matumaini ya kudumu kwamba, kila kitu kinawezekana, ikiwa kama watu wataweka utashi na kuutekeleza utashi huu katika matendo.

Baba Mtakatifu alitembelea hata maeneo ambayo hapo mwanzoni yalionekana kuwa ni tete, akazungumza na watu bila wasi wasi, akaadhimisha Mafumbo ya Kanisa, watu wakaanza kuona mwanga mpya katika maisha yao, kiasi cha kuona ushuhuda wa imani thabiti kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Ufunguzi wa Lango la huruma ya Mungu anakaza kusema Askofu mkuu Franco Coppola, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, limekuwa ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Hili limekuwa ni Lango la upendo, huruma, upatanisho, haki na msamaha, changamoto na mwaliko kwa wananchi wa Afrika ya Kati kutorudia tena huko walikotoka kwani wakifanya hivyo watageuka kuwa ni nguzo ya chumvi! Wananchi waendelee kujenga upendo na mshikamano, kwa kufahamiana na kuthaminiana; kwa kusaidiana na kushirikiana. Wanasiasa pia waoneshe ukomavu na utashi wa kisiasa kwamba, wanataka kuleta mabadiliko na kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha ya wananchi wa Afrika ya kati.

Kuna mwamko mpya, hata kampeni zimeendeshwa kwa ustaarabu, kwa kuonesha kamba, wanataka kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa. Changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, silaha ambazo zimezagaa mikononi mwa wananchi zinarudishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalam, ili amani, ustawi na maendeleo ya wengi viweze kutawala. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutoa msaada wa hali na mali, ili kuhakikisha kwamba, Serikali mpya itakaoundwa huko Afrika ya Kati inatekeleza vyema dhamana na majukumu yake anasema Askofu mkuu Franco Coppola, Balozi wa Vatican nchini Afrika ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.