2016-01-04 07:50:00

Vijana wa Ulaya kukutana mjini Riga, Lithuania kunako mwaka 2017


Vijana wa Jumuiya ya Taizè kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya wamehitimisha mkutano wao wa mwaka uliokuwa unafanyika huko Valencia, Hispania kuanzia tarehe 28 Desemba 2015 hadi tarehe 1 Januari 2016. Kwa mara ya kwanza mkutano huu utafanyika mjini Riga, Lithuania kuanzia tarehe 28 Desemba 2016 hadi tarehe 1 Januari 2017. Ni matumaini ya Fra Alois kwamba, hija ya vijana wa Ulaya itasaidia mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa Bara la Ulaya licha ya tofauti zinazojitokeza. Mkazo ni umoja na mshikamano kati ya nchi za Ulaya na kati ya Ulaya na Mabara mengine duniani.

Vijana wanachangamotishwa kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa umoja, upendo, mshikamano na amani, ili maisha yao yaweze kung’aa katika giza la hofu na mashaka, vita na kinzani linaloendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Ushuhuda wao unaweza kuonekana kuwa kama nyota inayofifia, lakini ni muhimu sana kwa ushuhuda wa watu wa nyakati. Vijana hawa watakwenda Cuba mwezi Februari 2016 ili kuanzisha Jumuiya ya Taizè, ili kupandikiza mbegu ya ukarimu na mshikamano.

Fra Alois anaendelea kusema kwamba, kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe Mei, Mosi, 2016 vijana 150 watakwenda Bucarest, Romania, ili kuadhiadhimisha Siku kuu ya Pasaka na waamini wa Kanisa la Kiorthodox, kama kielelezo cha kukoleza majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika uhalisia wa maisha. Vijana wa Taizè huko Valencia, Hispania wametafakari kuhusu ukarimu, kiasi, amani pamoja na changamoto zinazoendelea kuwaandama binadamu katika ulimwengu mamboleo, hususan wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.

Vijana wamekumbushwa kwamba, Mungu ni upendo, kumbe hakuna sababu ya kuendekeza vita, migogoro na kinzani, mwaliko kwa vijana kuwa kweli ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano; mambo ambayo yanapaswa kushuhudiwa si kwa maneno bali kwa njia ya matendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Huu pia ni mwaliko kwa vijana kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa ambalo ni moja chini ya Kristo mchungaji wake mkuu.

Vijana wasimame kidete kushuhudia ukarimu kwa wale wanaohitaji msaada; kuwalinda na kuwatetea wote wanaonyanyaswa na kudhulumiwa pamoja na kuwashirikisha wengine karama na mapaji ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Vijana wakuze na kudumisha moyo wa sala na tafakari ya Neno la Mungu ambalo ni dira na mwongozo wa maisha yao ya kiroho.

Wakati huo huo, Kardinali Antonio Canizares Llovera, amewapongeza vijana wakiokuwa wanahudhuria mkutano wa Taizè huko Valencia na kuwaalika kumkimbilia Kristo Yesu, ili aweze kuwakirimia uhuru wa kweli, utimilifu wa maisha pamoja na kukata kiu yao ya udadisi kuhusu maisha ya Kikristo. Yes uni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele, hapa vijana wanaweza kutua nanga ya matumaini ya maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.