2016-01-04 15:37:00

Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa katika kulinda na kudumisha familia


Padre Tumaini Litereku Ngonyani  kutoka Jimbo kuu la Songea, Tanzania ambaye kwa sasa anaendelea na masomo yake ya juu nchini Ujerumani katika mahojiano maalum na Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ushuhuda wa Injili ya familia anasema, familia zinapaswa kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu iliyosimama kidete kuhakikisha kwamba, inatekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake, licha ya shida, magumu na changamoto zilizojitokeza.

Padre Ngonyani anakaza kusema, Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa na akina baba wa familia, kwa kuonesha upendo wa dhati, kwa kujali na kuwajibika vyema katika utekelezaji wa majukumu mbali mbali ya maisha na utume wa familia. Mtakatifu Yosefu ni shuhuda na mfano wa Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Ni Baba aliyejinyima mambo mengi, akajisadaka kwa ajili ya ulinzi, usalama, ustawi na maendeleo ya Bikira Maria na Mtoto Yesu.

Padre Ngonyani anatawaka mababa wa familia kuwa na msimamo thabiti katika maisha na utume kwa familia; kwa kuwalinda, kuwalea na kuwahudumia watoto wao ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kamwe wasichoke kujisadaka wala kukata tamaa kutokana na magumu wanayokabiliana nayo, ili kuhakikisha kwamba, wanaambata huruma, upendo na msamaha, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kamwe baba wa familia wasiwe na kishawishi cha kutaka kupata faraja nje ya familia zao, huko watajichumia majanga yatakayoisambaratisha familia. “Michepuko” haina tena deal” wanasema waswahili. Mtakatifu Yosefu alipambana kiume ili kuhakikisha kwamba, anaipenda, anailinda na kutunza Familia takatifu. Akahakikisha kwamba, familia yake inaishi kadiri ya mpango wa Mungu kwa kuzingatia haki msingi za binadamu.

Baba wa familia ni kichwa na kiungo muhimu sana cha familia, kumbe anapaswa kuwa na msimamo thabiti katika maisha ya kifamilia, akiongozwa na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari kutangaza na kuishuhudia Injili ya familia, ikimwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji! Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, Mwaka wa Familia nchini Tanzania pamoja na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ziwe ni fursa za kuendelea kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari kucharuka kushuhudia Injili ya familia inayoambata huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.