2016-01-04 07:41:00

Mfungulieni Kristo Malango ya maisha yenu!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili ya pili ya Kipindi cha Noeli, hapo tarehe 3 Januari 2016 amegusia kuhusu Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuwapatia watu nafasi ya kumsikiliza, kumfahamu na hatimaye kugusa na kuonja upendo wa Mungu Baba. Neno wa Mungu ni sawa na Mwana wa pekee wa Mungu, aliyefanyika mwili, utimilifu wa upendo na uaminifu, huyu ndiye Yesu Kristo.

Mwinjili Yohane anasema Neno wa Mungu alikuja kwa watu wake, lakini kwa bahati mbaya hawakumpokea. Neno wa Mungu ni mwanga, lakini watu wakapenda kutembea zaidi katika giza, kiasi hata cha kufunga mlango mbele ya uso wa Mwana wa Mungu. Hapa fumbo la ubaya linaendelea kushamiri katika miyo ya watu, mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa macho ili kamwe ubaya usitawale, kwani daima ubaya uko mlangoni pa maisha ya binadamu. Ole wake mtu yule atakaye ruhusu ubaya uingie ndani mwake, kwani atajikuta akijifungia katika ubinafsi wake.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kufungua malango ya mioyo yao, ili Neno wa Mungu ambaye ni Kristo Yesu, apate kuingia, ili kuweza kufanyika kuwa ni watoto wake. Mama Kanisa anawahimiza watoto wake kupokea Mwanga ambao kimsingi ni Neno la uzima katika maisha yao. Ikiwa kama waamini watakuwa na ujasiri wa kumpokea Yesu katika maisha yao, watajifunza kuwa ni watu wenye huruma kama alivyo Yeye. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha Injili ili iweze kuwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kusikiliza, kujisomea, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika  maisha ya kila siku, kama sehemu ya mchakato wa kutaka kumfahamu Yesu zaidi, tayari kumpeleka kwa watu wengine. Huu ndio wito na furaha ya kila Mkristo, yaani kumwonesha Yesu na kumtoa kwa wengine.

Uwepo wa Yesu unawalinda waja wake na ubaya pamoja na shetani ambaye daima anarandaranda kwenye milango ya maisha na mioyo ya waamini akitaka kuingia. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiaminisha kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Yes una Kanisa na kuendelea kumtafakari mbele ya Pango la Mtoto Yesu, wakati huu wa Kipindi cha Noeli.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu amewatakia waamini wote amani na salama wakati huu wa mwanzo wa Mwaka Mpya wa 2016. Hata katika nyakati za majonzi na masikitiko, waamini wasiogope kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ni chemchemi ya huruma na matumaini yao. Waamini wanakumbushwa kusinda kutojali na kuambata amani; changamoto na mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha kauli mbiu hii katika maisha yao ya kila siku. Anawatak waamini kujenga utamaduni wa kujisomea, Neno la Mungu katika maisha yao, ili waweze kumfahamu Yesu vizuri zaidi pamoja na kuwasaidia wengine kumfahamu vyema. Waamini wawe na mazoea ya kutembea na Biblia katika mifuko na mikoba yao, ili kujisomea sehemu ya Maandiko Matakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.