2016-01-02 12:16:00

Watumishi wa umma Tanzania watakiwa kutumia mawasiliano ya barua pepe serikalini


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga marufuku matumizi ya Barua pepe za kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au kupokea taarifa za Serikali na kuwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo rasmi wa Mawasiliano ya Barua Pepe Serikalini (GMS) ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha mawasiliano kwa njia ya Mtandao. Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angella Kairuki alipokuwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao (e Government Agency) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji na ufanisi wa matumizi ya TEHAMA Serikalini.

“Sasa kuna watumishi 7, 000 wanaotumia anwani za Barua pepe za Serikali, idadi hii ni ndogo lazima iongezeke, hatuwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa taarifa za Serikali kwa kutumia Barua Pepe nje ya mfumo huu” Amesisitiza na kuongeza kuwa Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye mawasiliano binafsi. Amesema kwa kutambua umuhimu wa uimarishaji wa mawasiliano ya TEHAMA Serikalini na kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia mitandao mbalimbali ipo haja ya kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia Barua Pepe za Serikali.

Mhe. Kairuki amewataka watendaji wa Wakala hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia uratibu wa zoezi hilo ili kuhakikisha kuwa Wizara, Idara na Taasisi zote za umma zinaunganishwa na mfumo rasmi wa Serikali ili kuwa na mfumo mmoja wa Mawasiliano. “Katika hili ninatoa siku 60 mhakikishe kuwa mnakamilisha kwa Taasisi zilizobaki ili kwa wale watakaopuuzia hatua zianze kuchukuliwa”Ameeleza Mhe. Angella. Aidha, ametoa wito kwa watendaji wa Wakala hiyo kuweka mpango wa kuwawezesha na kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi waliopo kazini kwa kujenga utaratibu wa kuwarithisha uzoefu watumishi ili kuendelea kuimarisha ufanisi na utendaji wa Wakala hiyo.

Mhe. Kairuki amewataka kuwa wabunifu katika kuanzisha mifumo mipya ya TEHAMA ili kuimarisha dhana ya Serikali mtandao ili kupunguza gharama hadi kufikia asilimia 5 ya fedha zinazotumika kuendeshea masuala mbalimbali ambayo yangefanywa kupitia matumizi ya TEHAMA.  Akizungumzia kuhusu ununuzi wa vifaa vya TEHAMA serikalini ameitaka Wakala hiyo kutoa ushauri ili kudhibiti mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha katika kununulia vifaa hivyo kwa gharama kubwa wakati vinaweza kupatikana kwa bei ya kawaida.

“Katika hili Serikali itachukua hatua kwa yeyote atakayebainika katika upotevu wa mapato mhakikishe mnazisaidia Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika masuala ya ununuzi wa mifumo na vifaa vya TEHAMA ili mifumo inayonunuliwa iwe na manufaa kwa wananchi na thamani halisi ya fedha”  Amesema Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa huduma kupitia mtandao ili wananchi waweze kupata huduma hizo mahali walipo kwa gharama nafuu na kutoa wito kwa watumishi wa Wakala ya Serikali mtandao (e-Gov) kuwa wabunifu katika kutengeneza programu mbalimbali na mifumo salama itakayowasaidia wananchi kupata huduma.

Aidha, katika hatua nyingine ameitaka e-Gov kuendelelea kujenga uwezo katika kudhibiti dharura na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza katika matumizi ya TEHAMA na kuitaka Wakala hiyo iendelee kulifanyia kazi suala la kuwezesha mifumo ya Serikali kuzungumza kati ya taasisi moja hadi nyingine ili huduma zote ziweze kupatikana katika eneo moja na kuondoa urudufu wa mifumo iliyopo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (e-Gov) Dkt. Jabiri Bakari akitoa taarifa ya utendaji wa Wakala hiyo amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali toka kuanzishwa kwake Julai 11, 2012 imeendelea kupata ufanisi katika uimarishaji wa Serikali Mtandao. Amesema kuwa Wakala hiyo inaendelea kuhakikisha kuwa huduma za Serikali zinawafikia wananchi kupitia mtandao mahali walipo na kuhakikisha kuwa inafanikisha lengo la huduma zote za Serikali kupatikana chini ya dirisha moja. Aidha amesema kuwa Wakala ya Serikali Mtandao itaendelea kuhakikisha kuwa usimamizi wa viwango vya matumizi ya TEHAMA katika Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali vinazingatiwa.

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.