2016-01-02 16:12:00

Itifaki kati ya Palestina na Vatican yaanza kutekelezwa!


Itifaki ya makubaliano kati ya Vatican na Taifa la Palestina iliyotiwa sahihi na pande hizi mbili kunako tarehe 26 Juni 2015, baada ya kukamilisha maridhiano yote, kuanzia tarehe 2 Januari 2016 imeanza kutumika kadiri ya kipengele namba 30 cha itifaki hii. Itifaki imegawanyika katika ibara 32 zinazoundwa na sura 8 zenye utangulizi, zinazoonesha mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa nchini Palestina.

Itifaki hii inakazia pamoja na mambo mengine, suluhu ya amani kwa njia ya majadiliano ili kusitisha vita ambayo imeendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao kwenye Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Itakumbukwa kwamba mchakato wa itifaki hii ulianza kunako tarehe 15 Februari 2000 baada ya majadiliano yaliyofanyika kati ya tume ya pamoja ya Vatican na Serikali ya Palestina. Itifaki hii ikatiwa sahihi mjini Vatican hapo tarehe 26 Juni 2015 na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Bwana Riad Al- Malki, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Serikali ya Palestina, alitia mkwaju kwenye itifaki hii kwa niaba ya Serikali yake. Tukio hili la kihistoria, lilihudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu kutoka Vatican na Serikali ya Palestina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.