2015-12-31 08:53:00

Wahudumu wa Injili 22 wameuwawa kikatili katika mwaka 2015


Katika kipindi cha mwaka 2015 kuna wahudumu wa Injili 22 waliouwawa kikatili sehemu mbali mbali za dunia, kati yao kuna Mapadre 13, watawa 4 na walei 3 na kwamba, katika kipindi cha miaka saba mfululizo, Amerika ya Kusini inaendelea kushika nafasi ya kwanza kwa mauaji ya Mihimili ya Uinjilishaji, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari za Kimissionari, Fides. Takwimu zinaonesha kwamba, huko Amerika ya Kusini viongozi wa Kanisa 8 wameuwawa. Barani Afrika kuna Mapadre watatu, mtawa mmoja na mlei mmoja. Bara la Asia linashikilia nafasi ya tatu kwa mauaji ya Mihimili ya Uinjilishaji kwa kuwauwa viongozi 7 na hatimaye, Ulaya imeshuhudia Mapadre wawili wakiuwawa kikatili huko Hispania.

Taarifa za Fides zinaonesha kwamba, viongozi wengi wa Kanisa wameuwawa katika majaribio ya ujambazi na wizi wa kutumia nguvu. Hizi ni dalili za kumong’onyoka kwa maadili na utu wema; kuongezeka kwa umaskini na hali ngumu ya maisha: kiuchumi, kijami na kitamaduni, kiasi cha watu kutafuta njia ya mkato kwa kujiingiza katika magenge ya wezi na wanyang’anyi. Haya ni matukio ambayo yanakumbatia utamaduni wa kifo kwa kutothamini Injili ya uhai, ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hakuna awaye yote anayepaswa kuwapokonya wenzake!

Mapadre, Watawa na Walei waliouwawa ni mashuhuda wa Injili ya mshikamano na mapendo, waliokuwa wanatangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya huduma za kichungaji katika maeneo yao pamoja na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Kwa upande wake, Padre Vito Del Prete, mmissionari anakaza kusema, matukio ya mauaji, dhuluma na nyanyaso kwa viongozi wa Kanisa yanaendelea kuongezeka maradufu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kuonekana kuwa ni sehemu ya utandawazi usiojali mateso na mahangaiko ya wengine. Haya ni mashambuli na mauaji yanayofanywa kwa ngazi ya kimataifa na vikundi kama vile vya Boko haram, Isis na Al Shabab.

Katika mwelekeo kama huu, waamini wanaalikwa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake! Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na watu wote wenye mapenzi mema ili kujenga Jamii inayojikita katika haki, amani, upendo na mshikamano. Ikumbukwe kwamba, kuna viongozi wengi wa Kanisa wanaoendelea kujisadaka kwa hali na mali, kiasi hata cha kuishia kama mshumaa uliosahaulika makaburini! Lakini bado wanashuhudia Injili ya upendo na huduma kwa Familia ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.