2015-12-31 09:55:00

Kigoda cha Kardinali Laurent Monsengwo chazinduliwa DRC


Katika mchakato wa uzinduzi wa mwaka wa masomo kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Yohane XXIII, iliyoko nchini DRC, kumeanzishwa “Kiti cha Kardinali Laurent Monsengwo” kinachopania kutoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu, ili kuimarisha tunu msingi za kimaadili, kiutu na kiroho. Hizi ni juhudi za ushirikiano na Chuo kikuu cha Kikatoliki Congo. Kiti cha Kardinali Monsengwo kitakuwa chini ya Professa Jean Gèrard Baende.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa “Kiti cha Kardinali Laurent Monsengwo”, Professa Baende amekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha sekta ya elimu kwani utajiri wa kwanza unaofumbatwa katika nchi yoyote ile ni rasilimali watu! Kanisa linapenda kuwekeza katika majiundo makini ya watu: kiroho na kimwili, ili kusaidia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu sanjari na kuchangia maendeleo ya watu katika sekta mbali mbali za maisha ya kijamii.

Professa Baende anakaza kusema, misingi ya demokrasia na utawala bora haina budi kukuzwa na kudumishwa kwa kukazia uhuru, haki msingi za binadamu; utawala wa sheria na uhuru wa mawazo; maboresho katika huduma za kijamii na ushiriki wa wananchi katika kuamua, kupanga na kutekeleza mikakati ya maendeleo; ukweli na uwazi; kasi na ufanisi katika utekelezaji wa sera na mikakati iliyobuniwa na Jamii husika. Haya ni mambo ambayo wanasiasa wanapaswa kuyazingatia ili demokrasia na utawala bora viweze kushamiri kati ya watu wao.

Kanuni maadili na utu wema ni mambo msingi katika utekelezaji wa mchakato wa maendeleo ya wananchi wa DRC, kiroho na kimwili; mambo yanayojidhihirisha katika huduma bora ya elimu, afya na maendeleo; sanjari na kusimama kidete kulinda utu na heshima ya wanawake, ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo. Watoto wanapaswa kulindwa na kuhudumiwa, ili waweze kukua na kukomaa: kiroho, kimwili na kiakili bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa linapenda kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu kwa ajili ya wananchi wa DRC, ili kuwajengea uwezo wa kupambana na changamoto za kitaifa.

Kiti cha Kardinali Laurent Monsengwo pamoja na mambo mengine, kinalenga kufanya marekebisho katika mitaala ya ufundishaji katika shule za Sekondari, taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu, ili jamii iweze kuwafunda kwa kina na mapana wasomi wanaoweza pia kukabiliana na changamoto za kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.