2015-12-30 10:01:00

Vijana onesheni jeuri ya huruma ya Mungu katika maisha yenu!


Zaidi ya vijana elfu ishirini na tano wa Jumuiya ya Kieukumene ya Taizè kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya kuanzia tarehe 28 Desemba 2015 hadi tarehe Mosi, Januari 2016 wanakusanyika huko Valencia, Hispania ili kusali na kutafakari kuhusu ujasiri wa kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao. Imekuwa ni nafasi kwa viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wao kutoa salam za matashi mema kwa vijana hawa, ili kuwawezesha kuambata misingi ya haki, amani, upendo, udugu na maridhiano, ili kuwa kweli ni chachu ya mabadiliko katika ulimwengu ambamo kwa sasa umegeuka kuwa kama uwanja wa mapambano.

Fra Alois katika tafakari yake ya kwanza kwa vijana hawa amegusia kiu ya watu kutaka kuona haki, amani na maridhiano vinatawala huko Mashariki ya kati. Hii ni fursa kwa vijana wa kizazi kipya Barani Ulaya kufungua masikio na mioyo yao tayari kusikiliza kilio cha wahamiaji na wakibizi wanaotafuta usalama na uhakika wa maisha bora Barani Ulaya. Ni nafasi ya kuangalia athari za mabadiliko ya tabianchi, vita na majanga asilia, mambo ambayo yanagusa akili na mioyo ya wengi, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu.

Katika ulimwengu ambamo woga na wasi wasi vinaendelea kutawala kutokana na vita pamoja na vitendo vya kigaidi, vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu, hapo kuna haja ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu. Hii ni changamoto kwa binadamu kujipatanisha na Mungu, jirani pamoja na mazingira, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Familia ya binadamu hapa duniani inapaswa kutembea kwa matumaini, lakini kwa sasa watu wengi wamekosa matumaini na matokeo yake woga na wasi wasi vinatawala katika akili za watu!

Fra Alois anakaza kusema, katika kipindi cha miaka mitatu, Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè itaongozwa na maneno makuu matatu: furaha, kiasi na huruma. Hija ya Jumuiya hii itaanza mapambazuko ya mwaka 2016 kwa huruma, changamoto makini inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Watu watambue na kukimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao kwani Mungu yuko tayari kuwapokea na kuwajalia msamaha, amani na utulivu wa ndani.

Changamoto ya pili wanayotaka kuifanyia kazi ni msamaha, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni chombo cha msamaha na huruma ya Mungu, hivyo basi waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maeneo yao. Kwa ufupi, msamaha huu unaweza kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kuonesha moyo wa huruma na mapendo.

Tatu, vijana wanapaswa kuonesha umoja na mshikamano na watu wanaoteseka kutokana na hali mbali mbali za maisha na kwa njia hii, kweli wanaweza kuleta mabadiliko katika ulimwengu huu ambao kwa sasa unaonekana kumezwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kama anavyokaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko. Nne, vijana wawe wepesi kumwilisha huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii, kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wahamiaji na wakimbizi .

Tano, huruma ya Mungu ijioneshe kwa namna ya pekee, kwa vijana kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, chemchemi ya haki amani na maridhiano kati ya watu. Vijana waoneshe utamaduni wa kuwa na kiasi katika maisha yao na kwa kufanya hivi, wataweza kuwa kweli ni chemchemi ya furaha ya maisha. Utu wa mtu ni muhumu sana kuliko hata vitu alivyo navyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.