2015-12-30 11:33:00

Uchu wa mali na madaraka ni sababu kubwa za machafuko ya kisiasa Barani Afrika


Haki, amani na upatanisho ni fadhila zinazositawi pale tu utu, heshima na mafao ya wengi yatapewa kipaumbele cha pekee kwa kujikita katika maridhiano kwa kuheshimu maisha ya binadamu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Majadiliano katika ukweli na uwazi sanjari na utawala bora unaozingaria Katiba na Sheria za nchi ni mambo muhimu sana katika kudumisha amani.

Lakini kwa bahati mbaya, amani Barani Afrika inaendelea kuwa ni ndoto kwa watu wengi kutokana na baadhi ya viongozi wa kisiasa kupindisha katiba za nchi kwa kumezwa mno na uchu wa madaraka na mali; matokeo yake ni vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii inayozalisha makundi makubwa ya wahamiaji, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi zao wenyewe! Kuna baadhi ya viongozi wamejiimarisha kisiasa na kiuchumi kwa kutumia ukabila na udini usiokuwa na mvuto wala mashiko na matokeo yake ni maafa ya watu wasiokuwa na hatia!

Viongozi wa kisiasa wanapaswa kutambua kwamba, uongozi ni huduma inayojikita katika kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uchu wa madaraka na tabia ya baadhi ya viongozi kubadilisha na kupindisha Katiba ili kuendelea kubaki madarakani kumekuwa ni chanzo cha maafa ya watu wasiokuwa na hatia sehemu mbali mbali Barani Afrika. Ni maneno ya Askofu mkuu Jacob Chimeledya Mkuu wa Kanisa Anglikan Tanzania katika mahubiri yake hivi karibuni huko Mpwapwa, Dodoma.

Uchu wa mali na madaraka miongoni mwa wanasiasa na wapambe wao, imekuwa ni chanzo cha vurugu na maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Hawa ni viongozi waliopewa dhamana na wananchi ili kuwaonesha njia, lakini baadaye wakageuka “Mbogo” kwa kutaka kung’ang’ania madarakani hata pale muda wao wa uongozi unapofikia ukomo. Hizi ni dalili za ubinafsi na uchoyo kwa viongozi kama hawa na matokeo yake hali ya maisha inadidimia, gharama ya maisha inapanda na hapo wananchi wa kawaida wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma msingi za elimu, afya, miundo mbinu na maendeleo endelevu!

Askofu Chimeledya ameutaka Umoja wa Afrika kuongeza juhhudi katika kutatua migogoro ya kivita na kinzani za kisiasa, ili amani, utulivu na ustawi viweze kurejea Barani Afrika, tayari kucharuka kwa maendeleo sanjari na kuokoa maisha ya watu pamoja na kutunza mazingira. Hali ya kisiasa nchini Burundi na DRC badi ni tete; Rwanda imebadili Katiba ili kutoa nafasi kwa Rais aliyeko madarakani kuendelea kuongoza kwa awamu tatu mfululizo. Tabia kama hizi ndizo zinazosababisha majanga ya kijamii.

Tanzania licha ya kasoro za mara kwa mara katika chaguzi zake, bado inaendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kuachia madaraka kwa amani na utulivu na Marais wastaafu kuendelea kushiriki katika ujenzi wa nchi yao. Tangu kung’atuka kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere, kumekuwepo na utamaduni mzuri wa kuachiana madaraka, hadi wakati huu, Dr. John Pombe Magufuli ameshika hatamu za uongozi, kwa mwendo mdundo! Yaani hapa ni kazi tu!

Ni kiongozi ambaye ameanza kujipambanua kwa kukazia kanuni maadili, utawala wa sheria, haki na amani pamoja na kutoa kipaumbele cha pekee katika kutatua kero za watanzania wengi. Saratani ya rushwa inaonekana kana kwamba, imeaanza kupata tiba, Serikali ya awamu ya tano ikipewa ushirikiano wa dhati, Tanzania itaandika ukurasa mpya wa maendeleo na kuondoka kwenye orodha ya omba omba! Hapa watanzania wanapaswa kufanya kazi kwa kujituma, kwa juhudi na maarifa. Haki, amani na maridhiano kati ya watu yanaweza kupatikana, ikiwa kama kila mwananchi atatekeleza dhamana na wajibu wake barabara, kwa kuzingatia utawala wa sheria, utu na heshima ya binadamu. Watu wajenge utamaduni wa kuthaminiana na kuheshimiana anasema Askofu mkuu Jacob Chimeledya, Mkuu wa Kanisa Anglikan, nchini Tanzania.

Na Rodrick Minja,

Mpwapwa, Dodoma. Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.