2015-12-30 08:45:00

Papa Francisko kwa mwaka 2015 amesimama kidete kutetea mazingira na amani


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume juu ya Sifa kwako utunzaji Bora wa mazingira, nyumba ya wote, Laudato si anasema hii ni changamoto pevu katika familia ya binadamu kwani inajikita katika haki msingi za binadamu sanjari na udumishaji wa amani, ustawi na maendeleo ya binadamu wote. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha umaskini mkubwa kwa watu sehemu mbali mbali za dunia, lakini waathirika wakuu ni wale akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.

Hapa kuna haja anasema Baba Mtakatifu ya kuwa na mwelekeo sahihi wa kiekolojia, watu kuwajibika pamoja na kujenga mfumo wa sheria utakaohakikisha usalama wa mifumo ya mazingira. Kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote sanjari na kuzingatia sheria asilia. Jamii pia zinapaswa kulinda na kudumisha utamaduni wa watu mahalia. Jumuiya ya Kimataifa ijenge utamaduni wa kujadiliana, kuweza kuamua na kutenda kwa kushirikiana kwa ajili ya mafao ya wengi. Juhudi zote hizi hazina budi kwenda sanjari na elimu makini juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Kwa ufupi huu umekuwa ni mchango mkubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2015, mwaka ambao umewakutanisha “vigogo” wa dunia huko Paris, Ufaransa ili kujadili na hatimaye kupitisha sera na mikakati ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha utashi wa kisiasa na mshikamano wa kimataifa unaojikita katika kanuni auni kama sehemu ya utekelezaji wa maamuzi magumu yaliyofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa huko Paris, Ufaransa.

Askofu Mario Toso wa Jimbo la Faenza Modigliana, Italia, ambaye hadi kuteuliwa kwake hivi karibuni alikuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha mwaka 2015 amechangia kwa namna ya pekee watu kuona umuhimu wa kutunza mazingira kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, maendeleo na mafao ya wengi.

Hii inatokana na ukweli kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi zimeitikisha Jumuiya ya Kimataifa pasi na ubaguzi, lakini waathirika wakubwa ni nchi maskini. Hapa kuna haja ya kuwa na toba na wongofu wa kiekolojia, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu sanjari na kuondokana na ubaguzi unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Hapa mkazo unapaswa kuwa ni udugu, uhuru, haki, amani na mafao ya wengi, mambo msingi katika kukuza na kudumisha amani duniani.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda uliokubaliwa wa kumwilisha na kushudia huruma ya Mungu inayojikita katika misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Waamini wawe wepesi kutenda mema kwa kutambua kwamba, Mungu ni chemchemi ya upendo, haki na msamaha. Waamini wakishaonja msamaha katika maisha yao, wanaweza pia kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Huruma ya Mungu iwe ni chachu ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mambo msingi katika kudumisha amani na ustawi wa wengi.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote anakazia kwa namna ya pekee utunzaji wa mazingira kama msingi wa kukuza na kudumisha amani. Athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia, zimekuwa ni sababu kubwa ya vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii na matokeo yake ni makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi; kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Kumbe, ikiwa kama kutakuwa na utunzaji bora wa mazingira, utawala bora, utu na heshima ya binadamu vikizingatiwa, amani inaweza kutawala katika akili na mioyo ya watu!

Baba Mtakatifu wakati wa hija yake Barani Afrika amekazia umuhimu wa kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho na maridhiano kati ya watu pamoja na kuwataka waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Waamini walei wanapaswa kuwajibika barabara katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao katika medani mbali mbali za maisha, ili kudumisha amani na mafungamano ya kijamii. Waamini washiriki kikamilifu katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma ya upendo kwa jirani anasema Askofu Mario Toso katika mahojiano maalum na Radio Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.