2015-12-29 07:43:00

Yaliyojiri katika maisha na utume wa Papa Francisko kwa Mwaka 2015


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; hija za kitume za Baba Mtakatifu Francisko sehemu mbali mbali za dunia; Sinodi ya familia na mchakato wa mageuzi ndani ya Sekretarieti ya Vatican ni kati ya mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2015. Hivi ndivyo anavyobainisha Askofu mkuu Angelo Becciu, Mwakilishi wa Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican.

Askofu mkuu Becciu anasema, aliguswa kwa namna ya pekee, pale Baba Mtakatifu Francisko alipomshirikisha nia yake ya kutaka kutangaza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hapa aliona ile furaha ya ndani kutoka kwa Baba Mtakatifu, kwani alitamani kuwapatia walimwengu nafasi ya kuweza kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao. Hapa Baba Mtakatifu akaonesha pia mwelekeo tofauti, ili kila mwamini na mtu mwenye mapenzi mema anayetaka kuambata huruma ya Mungu angeweza kuipata katika eneo lake na wala si lazima asafiri kwenda Roma.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huruma ya Mungu inapaswa kuwagusa watu wote bila ubaguzi, ndiyo maana ameamua kwamba, kuwepo na Malango ya huruma na upendo wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, ili kila mtu kadiri ya uwezo wake aonje na kuguswa na upendo wa huruma ya Mungu. Askofu mkuu Becciu anasema, hata yeye binafsi, mwaka huu unabaki kuwa ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wake.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia yameongozwa na kauli mbiu wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo. Kwa mara ya kwanza maadhimisho haya yamekazia kwa namna ya pekee dhana ya Sinodi, tangu maandalizi yake hadi maadhimisho yake. Hii ni changamoto mpya inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu hata pia kwa Makanisa mahalia, ili kupanga, kuamua na kutekeleza kwa pamoja mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima. Tofauti kabisa na maamuzi kufanywa na mtu mmoja au kikundi cha watu wachache ndani ya Kanisa.

Askofu mkuu Becciu anasema hii ni changamoto pevu kwa viongozi wa Kanisa waliozoea kufanya kazi kwa kutoa dira na mwelekeo pengine bila hata ya kuwahusisha wadau wengine katika maisha na utume wa Kanisa. Hapa Baba Mtakatifu anataka Kanisa kuhakikisha kwamba, linamwilisha sanaa ya majadiliano, umoja, upendo na mshikamano katika maisha na utume wa Kanisa. Hapa Halmashauri Walei katika ngazi mbali mbali zinapewa uzito wa pekee, ili kumwilisha tunu hizi msingi katika ujenzi wa Kanisa.

Baraza la ushauri ndani ya Jimbo lipewe pia kipaumbele cha pekee, kama ilivyo pia hata kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki au Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika ngazi za Kanda. Hapa kila mwamini anapaswa kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa na wala si mtazamaji au msikilizaji. Waamini washirikishwe kikamilifu katika mchakato mzima wa kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji.

Waamini wawe na ujasiri wa kushirikisha mawazo ya; wajenge utamaduni wa kusikiliza wengine na umakini wa kupokea mawazo ya wengine. Jambo la muhimu kwa Kanisa ni kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia waamini kupanga, kuamua na kutekeleza yote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo! Umoja, upendo na mshikamano unatambua pia nafasi ya kiongozi katika Kanisa, Jimbo, Parokia au katika Jumuiya husika. Kutokana na changamoto zote hizi, Askofu mkuu Becciu anakaza kusema, si rahisi kutekeleza changamoto hii, waamini wanapaswa kuonesha ujasiri na moyo mkuu, tayari kukumbatia mwelekeo huu mpya unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko.

Baba Mtakatifu Franciko anaendeleza nia ya kutaka kufanya mabadiliko msingi katika Sekretarieti kuu ya Vatican kama sehemu ya mchakato endelevu uliotolewa na Makardinali wakati wa mikutano yao elekezi, ili kweli Sekretarieti ya Vatican iwe ni kitovu cha Ukristo na Uinjilishaji wa kina, kwa kuwa na mwelekeo wa Kanisa la kiulimwengu sanjari na kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili, Kimaadili na Utu wema! Lengo ni kuhakikisha kwamba, Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudiwa sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Becciu anasema, katika mchakato wa kuleta mageuzi katika Sekretarieti kuu ya Vatican, Baba Mtakatifu anakumbana na vikwazo na changamoto mbali mbali, lakini amedhamiria kuhakikisha kwamba, lengo hili linatekelezwa kikamilifu pasi na wasi wasi wala woga wowote. Kashfa zilizojitokeza mjini Vatican, kamwe hazikumnyima Baba Mtakatifu Francisko usingizi na angependa kuona hatima ya kesi hii inayoendelea huko Mahakamani. Waandishi wa habari wanakumbushwa umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili, ukweli na uwazi pamoja na sheria.

Askofu mkuu Becciu anakaza kusema, ufunguzi wa Lango la Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Afrika ya kati ni kati ya picha ambazo zimenata na kuganda katika akili na moyo wake alipomwona Baba Mtakatifu katika hali ya unyenyekevu na ibada akifungua Lango la huruma ya Mungu, nje ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mara akakumbuka umuhimu wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuambata huruma ya Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha yao ndani ya Kristo.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, iligubikwa na mashaka makubwa, ikiwa kama Baba Mtakatifu angeweza kutekeleza nia hii njema! Familia ya Mungu nchini humo, ilipigwa na bumbuwazi, kuona nguvu ya imani iliyoshuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko kiasi cha kufanikiwa kwenda mjini Bangui pasi na wasi wasi, kama mjumbe wa haki, amani na upatanisho; huruma, upendo na maridhiano kati ya watu! Hii ndiyo zawadi kubwa ambayo Baba Mtakatifu ameiachia Familia ya Mungu nchini Afrika ya Kati, tayari kuandika ukurasa mpya unaojikita katika upendo wa huruma ya Mungu. Waamini waliguswa na Ibada zilizoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko kiasi cha kushuhudia ukelele wa furaha ukisikika kati yao! Wananchi wana kiu ya kuona haki, amani, msamaha, amani na utulivu vikitawala katika maisha yao ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.