2015-12-29 11:00:00

Wananchi 12, 222 wamekumbwa na Kipindupindu, kati yao 196 wamefariki dunia


Ugonjwa wa Kipindupindu bado unatishia maisha ya wananchi wengi nchini Tanzania, licha ya baadhi ya mikoa kuendelea kuudhibiti, lakini wananchi wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanazingatia ushauri wa wahudumu wa afya ili kutokomeza kabisa ugonjwa huu, ambao hadi kufikia tarehe 28 Desemba 2015 watu 12, 222 walikuwa wameambukuzwa ugonjwa huo na wagonjwa 196 wamekwisha fariki dunia. Lifuatalo ni Tamko la Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhusu hali ya ugonjwa wa Kipindu pindu nchini Tanzania.

Ninapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu hali ya ugonjwa wa kipindupindu ulioanza tarehe 15 Agosti, 2015 katika mkoa wa Dar es Salaam na kusambaa kwa kasi katika Mikoa mingine 21 ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na Pwani, Morogoro, Iringa, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma, Geita, Mara, Manyara, Arusha, Shinyanga, Tabora, Singida, Tanga, Lindi, Rukwa, Kagera, Katavi, Mbeya na Mwanza na Simiyu. Tangu ugonjwa huu uanze, jumla ya watu 12,222 wameugua Kipindupindu, na kati yao jumla ya watu 196 wameshafariki kwa ugonjwa huu ambayo ni sawa na asilimia 1.6 ya waliougua. Mkoa ambao umekuwa na wagonjwa wengi tangu mlipuko uanze ni Dar es Salaam 4,652 (asilimia 38 ya wagonjwa wote) ukifuatiwa na Tanga 1,470 (asilimia12), Singida 1016 (asilimia 8) Mwanza 909 (asilimia 7), Mara 804 (asilimia 7) na Arusha 756 (asilimia 7).

Ndugu Waandishi wa Habari,

Katika kipindi cha wiki mbili za kwanza za mwezi Desemba 2015, mikoa ya Mbeya (Kyela), Arusha (Arusha Mjini) na Mara (Musoma Vijijini) ilikuwa inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wapya wengi zaidi wa Kipindupindu. Kadhalika, mikoa ya Kigoma, Rukwa na Lindi ilianza kuripoti upya ugonjwa huu katika kipindi tajwa hapo juu. Aidha, Mikoa ya Tanga na Singida, ambayo hapo nyuma ilipata nafuu, sasa imeanza tena kuripoti ugonjwa huu. Hata hivyo, kasi ya ongezeko la ugonjwa imepungua katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Mbeya na Dar-es-Salaam kutokana na juhudi zinazofanywa na wadau ambao kwa pamoja, wameshirikiana kudhibiti ugonjwa huu kwa karibu zaidi. Aidha, mikoa ya Iringa na Kilimanjaro imefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu ambapo hakuna mgonjwa mpya kwa zaidi ya siku 30 zilizopita.

Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa mujibu wa taarifa ya tarehe 28 Desemba kumekuwa na wagonjwa wapya 76 na kufanya jumla ya wagonjwa wanaoendelea kupatiwa matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma katika mikoa yote iliyoathirika kuwa 115 na kifo kipya kimoja (1). Halmashauri inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi ni Morogoro Vijijini (12), Iramba (7), Simanjiro (7), Arusha Mjini (6) na Uvinza (4).  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Sekta nyingine husika, wadau wa maendeleo na wadau wengine inaendelea kukabiliana na ugonjwa huu kwa njia mbalimbali. Ofisi ya Rais iliitisha kikao cha pamoja katika ngazi ya Mawaziri na pia iliitisha kikao kingine kwa kushirikisha Wizara yangu, TAMISEMI, Wizara ya Maji, DAWASCO, DAWASA, Wizara ya Elimu na Sekretariat ya Mkoa wa Dar-es-Salaam. Lengo lilikuwa ni kupanga mikakati jumuishi na ya haraka itakayoweza kufanikisha udhibiti wa ugonjwa huu.

Kutokana na mwenendo wa mlipuko wa kipindupindu nchini, naendelea kusisitiza kuwa, maagizo niliyoyatoa tarehe 16 Desemba 2015 yazingatiwe na wananchi ili kudhibiti ugonjwa na kuokoa vifo vinavyotokana na ugonjwa huu. Maagizo haya ni pamoja na kunywa maji yaliyo safi na salama, kuepuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka:-

- kabla na baada ya kula

- baada ya kutoka chooni

- baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia

- baada ya kumhudumia mgonjwa

Aidha, ni muhimu kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, mabwawa na ziwani. Pia nasisitiza tena kuwa ni marufuku kuuza matunda yaliyokatwa na vyakula barabarani katika mazingira yasiyo safi na salama. Aidha, maagizo niliyoyatoa hapo awali kwa Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji ambao ni Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Maafisa Afya yaendelee kutekelezwa na kutolewa taarifa kwa wakati. Na kutokana na hili, nimeagiza kuandaliwa kwa taarifa ya mlipuko kwa kila wiki ili kupata hali halisi, na kila jumatatu wizara itatoa taarifa ya kila wiki ya ugonjwa.

Hitimisho

Kama nilivyosema hapo awali, kwa kuwa ugonjwa huu bado unaendelea kusambaa, mikoa ambayo bado haijaathirika ichukue hatua za tahadhari za kuzuia ili isipate mgonjwa yeyote wa Kipindupindu. Wizara itaendelea kufanya tathmini ya hatua zinazochukuliwa ili hatua stahiki zichukuliwe kuudhibti na kuutokomeza ugonjwa huu.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.