2015-12-28 15:41:00

Sala na Kazi ni chachu ya maendeleo kiroho na kimwili!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, tukingali bado shangweni wa Noeli, tunakusalimu kutoka katika Studio za Radio Vatican tukisema Tumsifu Yesu Kristo! Karibu tuendelee kuuadhimisha kwa pamoja mwaka wa Watawa duniani, kwa kuangazia uanzaji na ukuaji wa maisha ya kitawa ndani ya Kanisa. Kama tulivyokuahidi katika kipindi kilichopita; baada ya kutazama kwa uchache maisha ya kitawa yalivyo anza huko Jangwani Misri, leo tuangazie utawa ulivyoenea katika nchi za Magharibi. Tulikuahidi kukuletea habari kuhusu Mtakatifu Benedekto, tega sikio sasa, umfahamu Mtakatifu Benedikto.

Mtakatifu Benedikto alizaliwa huko Nursia, nchini Italia yapata mwaka wa 480. Alizaliwa katika familia bora, akiwa pacha na dada yake  Mt. Scholastica. Akiwa mvulana, aliishi Roma. Baadaye akaacha maisha ya kitaaluma, akaiacha nyumba ya baba  yake na utajiri wote, akiwa na lengo la kumtumikia Mungu tu. Hivyo akatafuta pahala ambapo angeweza kutimiza azma hiyo ya moyo wake. Akaweka makazi yake huko Enfide, karibu na Subiaco. Mara mmoja alikutana na Mtawa aliyeitwa Romanus, na huyo ndiye aliyepa vazi la Kitawa na kumshauri awe mtawa mheremita, yaani mkaa pweke. Aliishi katika hali hiyo kwa miaka mitatu, pasipo kujulikana na watu. Romanus alikuwa akimtembelea kwa siku maalumu na kumsaidia kwa mahitaji ya chakula na ushauri.

Katika kipindi hiki cha upweke huko utengoni, Benedikto alikomaa katika fadhila, alijifahamu mwenyewe binafsi, alikomaa katika ufahamu juu ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kama ilivyo kawaida, karama huwa haifichiki. Benedikto akajulikana na watu, wakaanza kumheshimu na kupenda kusikiliza busara zake. Baadaye akawa mtenda miujiza na watu wengi wakavutwa na fadhila zake na utakatifu wake; wakamfuata huko pangoni subiako ili awaongoze katika maisha ya kiroho.

Basi wafuasi hao akawajengea monasteri 12, na katika kila monasteri kulikuwamo na watawa 12 chini ya kiongozi mmoja, yeye mwenyewe aliishi katika monasteri ya 13, pamoja na watawa wachache, huku mwenyewe akiwa ndiye mkuu wa jumuia hiyo: akawafundisha kwa maneno na mfano wa maisha yake mwenyewe, lakini alikuwa ni Baba wa wamonaki wote. Wazo hili linaonekana wazi katika Kanuni yake sura ya kwanza, ambapo anachambua aina za wamonaki. Kutawa kisenobiti (yaani kutawa ndani ya jumuiya), Mt. Benedikto anaona ndiyo namna bora zaidi ya kuutafuta ukamilifu, kwa msaada wa watawa wengine ndani ya jumuiya, chini ya Kanuni na  kwa uongozi wa Abate.

Baada ya kuanzisha monasteri hizo, akaasisi pia shule kwa ajili ya watoto, ambamo baadhi ya wazaza walikuwa wanawatolea watoto wao kwa Monasteri, hivyo monasteri zikawa zinawaendeleza kwa kuwapa malezi-utu na malezi elimu. Miongoni mwao ni watakatifu Mauro na Placido.

Maisha ndani ya Jumuiya yanaongozwa kwa Kanuni maalumu. Hivyo aliandika Kanuni yake kwa Wamonaki, kanuni ambayo imekuwa na mchango mkubwa sana katika maisha si ya watawa tu, bali hata katika maisha ya watu wa Kawaida, na ndiyo maana baadaye Utawa wa Mtakatifu Benedikto umeheshimika katika kuchangia kwa kiasi kikubwa sana Ustaarabu wa Ulaya.

Kanuni yake ililengwa kwa walei wanaoyaacha malimwengu na kwa mwanga wa Injili kuishi maisha ya ufuasi wa Kristo. Na tunaona wazi kabisa Kanuni yake inalenga kumsaidia mtu kuutafuta ukamilifu wa maisha ya Kikristo. Anaongea mambo ya kawaida, ambayo mtu safi akiyafuata, hapo atakuwa anaimwilisha injili ya Kristo katika maisha halisia. Hilo linaonekana wazi sana katika sura ya Nne, ambapo anaongelea juu ya vyombo vya matendo mema. Anakazia pia maisha ya imani na fadhila mbalimbali zinazojengwa katika hofu ya Mungu. Ni kwa njia hiyo tunakuwa Wakristo kweli.

Jambo jingine la pekee sana katika Kanuni ya Mtakatifu Benedikto ni mkazo kuhusu Sala na Kazi. Mt. Benedikto hakuanzisha shirika lake ili kukidhi hitaji fulani katika kanisa kama yalivyoanzishwa mashirika mengine mengi. Alileta mtindo wa maisha ya pamoja, kumtafuta Mungu na kumtumikia ndani ya jumuiya. Hivyo kwa njia ya sala (ambayo anaitazama kama kazi ya Mungu), mtawa anayatakatifuza si maisha yake tu, bali maisha ya Kanisa na ya ulimwengu mzima. Ni kwa njia ya kazi, mtawa anajipatia chakula chake cha kila siku, na kwa ajili ya kuwalisha wahaji na wageni wanaofika monasterini. Kazi ya mikono kwa Mt. Benedikto ni namna bora sana ya kuitegemeza jumuiya na kuwasaidia wengine pia. Maisha ya kazi yalipewa msukumo wa pekee sana, huku uvivu na uzembe vikipigwa vita kali akisema “uvivu ni adui wa roho”.

Ni kwa kuunganisha hayo  mambo mawili, Ubenediktini ulisaidia katika kuleta maendeleo ya Ulaya wakati wa Karne za Kati. Na kwa nyakati zetu hizi, ubenediktini umesambaa ulimwengu mzima, na wanaendeleza maisha yayohayo ya kusali na kufanya kazi mbalimbali, ili kuchangia katika ukombozi wa mwanadamu kiroho na kimwili. Hivyo, Watawa Wabenediktini popote pale walipo, wanakushirikisha roho hiyo ya SALA na KAZI. Uwatafute, ukaangazwe zaidi.

Katika Afrika Mashariki, Ubenediktini umeota mizizi huko Peramiho – Songea, Ndanda – Mtwara, Hanga – Songea, Mvimwa – Sumbawanga, Imiliwaha, Chipole, Mpanda na Mwanza, (kwa upande wa Tanzania), na kwa upande wa Kenya, kuna Monasteri huko Tigoni, na huko Uganda, kuna monasteri huko Tororo. Katika sehemu hizo tajwa, ukijisikia wito wa Kitawa, unaweza kuandika Barua ya maombi kujiunga nao, ili nawe ukamtukuze Mungu kwa Sala na Kazi katika maisha ya jumuiya ya Kitawa. Hata waamini walei wanaweza kushiriki katika karama ya Mtakatifu Benedikto kama Waoblati (yaani utawa wa Tatu wa Mt. Benedikto). Yote waweza kuyapata kwa kuwatafuta sehemu hizo tajwa.

Katika sehemu hizo, watawa Wabenediktini pamoja na kuendesha maisha yao ya kitawa, wanatoa pia huduma za kijamii kwa watu kama vile Elimu, Afya, maji, nishati na barabara; wanasaidia watu katika maendeleo ya kilimo na mifugo; wanafanya shughuli za kichungaji katika maparokia, na wanaendesha vituo mbalimbali vya kiroho na kijamii; na ndivyo wanavyogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili, huku wakiyastaarabisha malimwengu kwa kazi zao na huduma zao.

Kutoka kwa Wabenediktini mpendwa msikilizaji, tujifunze Roho ya Kazi. Na hasa nyakati zetu hizi ambapo wapo watu wengi wanaopenda kuishi kwa kucheza bahati nasibu. Kazi ni kipimo cha utu, kazi ni afya, kazi ni heshima. Tufanye kazi kwa juhudi na maarifa ili tujipatia mahitaji ya kila siku sisi wenyewe na tujiletee maendeleo yetu sisi wenyewe. Nyakati zetu hizi ambamo kuna utamaduni uvivu ambapo watu wanapenda kuishi kwa kupiga domo na kulalamikalalamika tu bila kutimiza wajibu; tunahitaji kujenga nidhamu ya kazi. Katika nyakazi hizi ambamo watu wanapenda kufanya kazi kidogo sana au kwa muda mfupi sana na kukwapua lundo la malipo; tunahitaji kujenga dhamiri ya Kazi. Tufanye kazi halali, na tupokee malipo halali kwa kazi tuliyofanya. Ni hivyo tu, tutaleta maendeleo ya kweli.

Lakini pia Mt. Benedikto anakazia umuhimu wa Sala, ila siyo sala tu, sala na kazi. Hatuwezi kulala makanisani siku saba kwa saba, ili Mungu atufanyie miujiza ya maisha bora, haiwezekani! Mungu ametuumba kwa akili na utashi, na ametutuma kufanya kazi, kuutiisha ulimwengu. Tunatakiwa kusali, kuomba nguvu ya Mungu, kumshirikisha Mungu katika maisha na mipango yetu, huku sisi wenyewe tukitumia akili zetu, juhudi sahihi, na maarifa-fanisi katika kutekeleza mipango yetu. Hapo tutajijengea heshima, huku  Mungu akitukuzwa zaidi.

Basi mpendwa msikilizaji, hivyo ndivyo Mtakatifu Benedikto, Babu wa Umonaki wa Magharibi, na Msimamizi wa Ulaya, anavyopiga hodi nyumbani mwako akiwa na ujumbe wa SALA NA KAZI. Kukuletea habari hii kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Mtawa -  Mbenediktini, Padre Pambo Martin Mkorwe OSB, kutoka Mvimwa-Sumbawanga, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.