2015-12-28 07:22:00

Familia zinapaswa kujenga umoja, udugu na mshikamano wa dhati!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, katika Siku kuu ya Damilia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ameadhimisha pia Siku ya familia ndani ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu kwa kukumbusha kwamba, familia zinapaswa kuwa ni kitovu cha huruma na upendo wa Mungu na kwamba, Kanisa bado lina imani kubwa kwa familia katika maisha na utume wake!

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia anasema kumekuwepo na mwingiliano mkubwa kati ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia pamoja na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kanisa limetafakari kwa kina na mapana kuhusu wito na utume wa familia katika Kanisa na ulimwengu mamboleo. Kumbe, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwendelezo wa tafakari ya huruma ya Mungu inayopaswa kuwa ni dira na mwongozo kwa familia, tayari kufungua malango ya maisha na utume wao kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Askofu mkuu Paglia anakaza kusema, familia zinapaswa kumfungulia Mungu malango ya maisha yake ili kweli huruma na upendo wa Mungu viweze kuwasindikiza wanafamilia katika hija ya maisha yao ya kila siku. Familia za Kikristo ziwe ni mashuhuda wa matumaini kwa wale waliokata tamaa. Jubilei ya familia imekuwa ni ni fursa makini kwa Kanisa kuzikumbatia familia katika furaha, shida na matumaini.

Kanisa linatambua kwamba, kuna familia ambazo kweli ni mfano bora wa kuigwa, lakini pia kuna familia ambazo zimetikiswa katika maisha na kuachiwa majeraha makubwa, hizi pia zinapaswa kusaidiwa, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu. Mama Kanisa anapenda kukazia umuhimu wa familia zote, kujenga na kudumisha umoja, upendo na udugu, kwa kusaidiana kwa hali na mali. Kila familia ijisikie kuwa na wajibu wa kuambata huruma ya Mungu, ili nayo pia iweze kuwa kweli ni shuhuda ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Askofu mkuu Paglia anasema, maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita yamekuwa na mwitiko mkubwa kutoka ndani na nje ya Kanisa. Watu wengi wamechangia katika kujibu maswali dodoso, kwani familia ni msingi wa maisha ya kijami, hapa mwelekeo mkubwa ni mwitiko wa kibinadamu! Mchakato wa mabadiliko unaofanywa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo hauna budi kuzingatia pia utume na maisha ya familia ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.