2015-12-27 14:50:00

Papa Francisko atuma salam za rambi rambi kwa wananchi wa Ufilippini


Katika salam za rambi rambi zilizoandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko kwenda kwa Askofu mkuu Giuseppe Pinto, Balozi wa Vatican nchini Ufilippini, Baba Mtakatifu anasikitishwa sana na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa hivi karibuni huko Mindanao, Ufilippini na kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Baba Mtakatifu anaendelea kusali ili amani na utulivu viweze kupatikana katika eneo hili, ili kweli majadiliano, maridhiano na amani iwawezeshe watu kuishi kwa uhuru zaidi pasi na woga wala wasiwasi wa kushambuliwa. Baba Mtakatifu anawataka waamini wa dini mbali mbali nchini Ufilippini kukataa kishawishi cha kuwa na misimamo mikali na kuwashambulia wengine kwa kisingizio cha Mungu kwani Mungu ni upendo.

Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii kwa ajili ya kuwaombea neema na baraka wale wote walioguswa na kutikiswa na mashambulizi haya, ili waweze kupata faraja, huruma na nguvu ya kusonga mbele kwa matumaini zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.