2015-12-26 07:36:00

Noeli ya huruma ya Mungu kwa waja wake!


Kardinali Oswald Gracias, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mumbai anasema, Noeli ya Mwaka 2015 ni Noeli ya huruma ya Mungu, Siku kuu ambayo ikitumiwa vyema na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema inaweza kuleta mageuzi makubwa katika maisha na mioyo ya watu! Kardinali Gracias ameyasema haya hivi karibuni wakati alipokuwa anazindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na kwamba, Noeli ya mwaka huu ni tukio la neema na huruma ya Mungu katika maisha ya waja wake!

Yesu Kristo ndiye Lango kuu la huruma ya Mungu, ambamo waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kupitia wakiwa wametubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza kuandika kurasa mpya za maisha yao. Ikumbukwe kwamba, Huruma ni Mungu mwenyewe; ni Sura iliyofunuliwa kwa binadamu katika Agano la Kale na kupata utimilifu wake katika Agano Jipya kwa njia ya Yesu Kristo, Mwana wa Baba wa milele aliyezaliwa, akateswa, kufa na kufufuka kwa wafu, ili kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hatimaye, kuwajalia maisha ya uzima wa milele! Yesu ni kielelezo cha Umwilisho wa upendo na huruma ya Mungu unaoumba na kukomboa!

Kardinali Gracias anakaza kusema, dhana ya huruma ya Mungu imekuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa viongozi wakuu wa Kanisa kuanzia kwa Mwenyeheri Paulo VI, Yohane Paulo II, Papa mstaafu Benedikto XVI na kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko ambaye huruma ya Mungu ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuambata na kukumbatia huruma na upendo wa Mungu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Huruma maana yake ya ndani kabisa ni upendo wa dhati unaobubujika kutoka kwa Mungu mwenyewe ambaye kimsingi ni upendo kama anavyokaza kusema Papa Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume “ Deus caritas est” ambao, tarehe 25 Desemba 2015 unatimiza miaka kumi tangu ulipotolewa kwa mara ya kwanza, ukiwa ni Waraka wa kwanza kuandikwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Hapa waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanafungua akili na mioyo yao, tayari kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao, wakiwa tayari pia kuwashirikisha pia jirani zao. Waamini wajitaabishe kuwa ni wafuasi, wamissionari na vyombo vya huruma ya Mungu katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.