2015-12-25 09:11:00

Salam za Noeli kwa Roma na Ulimwengu: Urbi et Orbi!


Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi”, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushangilia siku ya wokovu wao, siku ya Bikira Maria; chemchemi ya matumaini mapya, amani, faraja, upendo na huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufungua mioyo yao kwa Yesu Kristo mwanzo mpya kwa maisha ya binadamu, ufunuo wa Huruma ya Mungu na mwanga unaofukuza giza, wasi wasi na majonzi na hivyo kuwakirimia watu amani inayowawezesha kukutana, kujadiliana na kupatana. Hii ni siku ya furaha kwa watu wote.

Hii ni Siku ya Bikira Maria, Mama wa Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu, akalazwa kwenye Pango la kulishia wanyama, kama ilivyokuwa kwa wachungaji kule kondeni, waamini pia wanaalikwa kwenda kuiangalia Ishara; tukio linalopyaishwa kila mwaka na Mama Kanisa; katika medani mbali mbali za maisha ya waamini wanaolipokea pendo la Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Kristo Yesu. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Kanisa pia linawaonesha  watu wote Ishara ya Mungu.

Mtoto aliyezaliwa ni Mwana wa aliye juu; Mkombozi wa ulimwengu, mwaliko kwa waamini kuabudu Wema wa Mungu uliofanyika mwili, hii ni changamoto kwa waamini kuacha wabubujike machozi ya toba ili kusafisha nyoyo zao! Yesu Kristo pekee ndiye anayeweza kumkomboa mwanadamu. Huruma ya Mungu peke yake ndiyo inayoweza kumwokoa mwanadamu kutoka katika ubaya unaomwandama kwa kufumbata ubinafsi. Neema ya Mungu inaweza kuleta wongofu wa mioyo kwa kufungua njia za ufumbuzi kwa masuala ambayo kibinadamu yanaonekana kana kwamba, yameshindikana.

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza, mahali anapozaliwa Mungu, hapo kunazaliwa pia: matumaini na amani na wala hakuna tena nafasi ya chuki na vita. Lakini kwa bahati mbaya hata mahali alipozaliwa Yesu Kristo bado kuna kinzani na vita na kwamba, amani inaendelea kuwa ni zawadi ambayo waamini wanapaswa kuendelea kuiomba na kudumisha. Baba Mtakatifu anaombea Israeli na Palestina ziweze kuanza tena majadiliano, ili kufikia muafaka utakaowawezesha wananchi wa Palestina na Israeli kuishi kwa maridhiano kwa kuvuka kinzani ambazo kwa muda mrefu zimewapambanisha na hivyo kuacha athari kubwa huko Mashariki ya kati.

Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu, ili muafaka uliopatikana huko kwenye Umoja wa Mataifa kuhusu usitishwaji wa vita huko Syria pamoja na kuwapatia msaada wa kiutu  viweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Makubaliano ya  kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa Libya, yaungwe mkono kwa kushinda utengano na mapambano ya silaha ambayo yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Jumuiya ya Kimataifa iendelee kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba mauaji ya watu wasiokuwa na hatia huko Iraq, Yemen na katika maeneo ya Kusini mwa Jangwa la Sahara yanasitishwa mara moja. Ni mauaji ambayo yamesababisha maafa, mateso na uharibifu mkubwa wa urithi wa kihistoria na kitamaduni kwa Jamii ya watu. Baba Mtakatifu anawakumbuka wale wote ambao wamekumbwa na vitendo vya kigaidi katika siku za hivi karibuni huko Misri, Beirut, Paris, Bamako na Tunisi.

Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za Noeli anawakumbuka Wakristo wanaoendelea kunyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani yao; Mtoto Yesu awajalie zawadi ya nguvu na faraja. Baba Mtakatifu anaendelea kuombea amani na maridhiano kwa wananchi wa DRC, Burundi na Sudan ya Kusini, ili kwa njia ya majadiliano, waweze kuimarisha juhudi za pamoja katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayojikita katika ari na moyo wa upatanisho na maelewano.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, Noeli ilete amani nchini Ukraine na faraja kwa wananchi walioathirika kutokana na vita; Noeli iwe ni chachu ya kutekeleza kwa vitendo makubaliano yaliyokwisha fikiwa, ili kudumisha amani katika Ukanda mzima. Furaha ya Siku kuu ya Noeli iangazie jitihada za wananchi wa Columbia, ili wakiwa wamehamasishwa na matumaini, wawe na ujasiri wa kusonga mbele na hamu yao ya kutaka kupata amani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mahali anapozaliwa Mungu, hapo kunazaliwa pia matumaini na watu wanathaminiwa utu wao. Hata leo hii kuna umati mkubwa wa watu ambao utu wao hautambulikani, kama ilivyokuwa kwa Mtoto Yesu. Hawa ni watu wanaoteseka kwa baridi, umaskini pamoja na kutengwa na jamii. Waamini waoneshe uwepo wao wa karibu kwa watu wasioweza kujilinda wenyewe, hususan watoto waliopelekwa vitani; wanawake wanaonyanyasika bila kuwasahau waathirika wa utumwa mamboleo pamoja na biashara haramu ya binadamu!

Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya faraja kwa watu wanaokimbia umaskini au vita; wanaothubutu hata kuhatarisha maisha yao. Wabarikiwe wale wote wanaowahudumia wakimbizi na wahamiaji kama mtu mmoja mmoja au kama taifa, kwa kuwasaidia kuanza ukurasa mpya wa maisha unaojikita katika utu kwa ajili yao wenyewe na ndugu zao. Baba Mtakatifu anawaombea matumaini wale wote ambao hawana fursa za ajira; Mwenyezi Mungu awasaidie viongozi wa kisiasa na kiuchumi, ili waweze kujikita katika mchakato wa kutafuta mafao ya wengi sanjari na kusimama kidete kulinda na kutetea utu wa kila binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, pale mahali ambapo anazaliwa Mwenyezi Mungu, hapo huruma inachipua na kustawi. Huruma ndiyo zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waamini na watu wote wenye mapenzi mema wakati huu wa Maadhimisho wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Waamini wanaalikwa kugundua upendo wa Mungu katika maisha yao. Mwenyezi Mungu awajalie wafungwa kuonja huruma na upendo wake unaoganga na kuponya madonda sanjari na kushinda ubaya.

Hivi ndivyo, Baba Mtakatifu Francisko anavyohitimisha salam za Noeli kwa mji wa Roma na ulimwengu katika ujumla wake, ”Urbi et Orbi” kwa kuwahimiza waamini washangilie Siku ya Wokovu wao. Kwa kutafakari Pango la Mtoto Yesu, wakaze macho yao kwenye mikono ya Yesu iliyofunguka na kuonesha huruma ya Mungu; wakati wanaposikiliza sauti ya Mtoto Yesu anayewanong’oneza ”kwa ajili ya ndugu na rafiki zangu ninasema: Amani iwe kwako!

Itakumbukwa kwamba, waamini waliojiandaa kikamilifu kwa kutimiza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa, wanaweza kujipatia rehema kamili wakati huu, Baba Mtakatifu anapotoa salam zake za ”Urbi et Orbi”. Mwishoni, amewatakia heri na baraka za Siku kuu ya Noeli waamini, mahujaji na wale wote waliokuwa wanafuatilia tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Noeli ya mwaka huu inaadhimishwa sanjari na Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuambata katika maisha yao huruma ya Mungu, ambaye ni Kristo Yesu, waliyopewa ili wao pia waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma kwa ndugu zao. Kwa njia hii amani itaweza kukua na kudumishwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.