2015-12-25 10:06:00

Familia ziwe ni shule na chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu!


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwendelezo wa mchakato wa Mama Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika huruma ya Mungu, mwaliko kwa familia kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha yake. Familia iwe ni mahali pa wongofu wa ndani, toba na msamaha; mahali pa ukarimu, upendo na huruma; ni mahali pa kujifunza kusamehe na kusamehewa, tayari kuambata huruma ya Mungu katika hija ya maisha.

Maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu kwa Mwaka 2015 yana umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anafanya tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Maadhimisho haya ni mwendelezo wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican kwa kutafakari: wito, utume na maisha ya familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko tangu alipozindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ameendelea kukazia umuhimu wa huruma ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuanzia ndani ya familia, kiini cha Uinjilishaji mpya. Kanisa halina budi kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu kwa kufungua malango yake, ili watu waweze kuingia na kujichotea baraka na neema zinazobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Familia na Kanisa ni taasisi mbili zinazokutana na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wake! Pasi na huruma, taasisi hizi mbili zinakosa dira na mwelekeo sahihi.

Lango la huruma ya Mungu liwasaidie wanafamilia kulinda, kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kukumbatia Injili ya uhai inayoshuhudiwa katika Injili ya familia dhidi ya utamaduni wa kifo na hali ya kukata tamaa inayoendelea kuiandama Familia ya mwanadamu. Yesu anasimama mlangoni akibisha, ikiwa kama familia zitakuwa tayari, zinaweza kumfungulia mlango, ili aweze kuandamana pamoja nao kwa njia ya Neno, Sakramenti na matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji!

Waamini wawe na ujasiri wa kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, ili nuru na mwanga wa huruma ya Mungu viweze kuondoa giza na makando kando yanayomwandama mwamini kiasi cha kushindwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Kwa njia hii, kweli familia zitakuwa ni chemchemi ya Injili ya familia na vyombo vya huruma ya Mungu. Mababa wa Sinodi ya Familia katika tamko lao, sehemu ya tatu, wanazihamasisha familia kuhakikisha kwamba, zinashiriki katika maisha na utume wa Kanisa kama mashuhuda wa Injili ya familia kwa zile familia zinazoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha.

Hapa familia zinahamasishwa kujenga utamaduni wa kimissionari, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na huruma ya Mungu kwa watu wanaokutana nao katika viunga vyao vya maisha. Jumuiya ya Kikristo iendelee kushikamana na familia katika utekelezaji wa mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita hasa katika ushuhuda wa maisha. Kwa kushirikiana na kushikamana, Kanisa kweli litaweza kusonga mbele na familia kuwa ni chachu ya Uinjilishaji mpya. Ukarimu, huruma, upendo, msamaha ni mambo msingi katika maisha na utume wa familia, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Familia zijenge utamaduni wa kumwilisha katika vipaumbele vyao matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama alivyofanya Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 18 Desemba 2015 kwa kufungua Lango la huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, Jijini Roma! Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, Jumapili tarehe 27 Desemba 2015, familia zitaanza maandamano kutoka kwenye Pango la Mtoto Yesu lililoko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na kupitia katika Lango kuu la Jubilei kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na huko ndani Baba Mtakatifu atawapokea na kuanza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu.

Hizi ni familia zinazoundwa na watoto, vijana, wazee na wagonjwa. Ni familia ambazo zimekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa bila kusahau familia ambazo zimeguswa na kutikiswa na madonda mbali mbali katika hija ya maisha yao. Hili ni tukio kubwa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Maadhimisho haya yawe ni ni mwendelezo wa hija ya maisha ya kiroho iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwataka waamini kuendelea kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia.

Maadhimisho haya yanamsaidia Baba Mtakatifu kuanza kuandika Waraka wake wa kitume mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, Waraka ambao utakuwa ni dira na mwongozo katika utekelezaji wa mikakati ya utume wa Familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo! Huu ndio mwelekeo unaopaswa kuoneshwa hata na Maaskofu mahalia katika Majimbo yao anasema Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia katika mahojiano maalum na gazeti la Avvenire, linalomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.