2015-12-24 09:40:00

Teknolojia ya habari ni changamoto na fursa hata kwa Mama Kanisa!


Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya jamii anabainisha kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari ambayo yamepelekea kuundwa kwa ulimwengu wa digitali ni changamoto kubwa na fursa makini kwa maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Uhai na Familia; Injili ya Imani na Matumaini.

Ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, Familia ya Mungu inaonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaopata chimbuko lake katika kweli za Kiinjili. Kwa ushuhuda huu, waamini wawasaidie Watu wa Mataifa wanaotaka kuonana na Yesu katika maisha yao hata kama hawataki kwenda Kanisa, ili waweze kukutana na miamba ya ushuhuda wa Injili ya Uhai, Familia, Imani na Matumaini, tayari kuwashirikisha katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Huu ni mwaliko wa kujenga, kudumisha na kuimarisha mshikamano wa udugu na upendo wa kweli kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, ili kuondokana na utandawazi usioguswa na mateso wala mahangaiko ya watu wengine. Hii ni changamoto endelevu iliyowahi kutolewa na Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake wa kitume Uinjilishaji Duniani, Evangelii Nuntiandi, kwa kusema kwamba, Kanisa halina budi kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko na wala si kwa njia ya propaganda za kidini.

Watu wa Mataifa waguswe na kuvutwa na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Na hii ndiyo nguvu ya Mama Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji anasema Askofu mkuu Claudio Maria Celli. Katika mapambazuko ya Karne ya ishirini na moja, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya habari, kiasi kwamba, leo hii, mtu anapata habari katika kiganja cha mkono wake, mahali popote pale alipo, hii ni ajabu na kweli

Lakini pamoja na maendeleo yote haya anasema Askofu mkuu Celli, Mama Kanisa bado anapaswa kuendelea kutumia njia za mawasiliano ya asili kama vile: Radio, Magazeti na Televisheni ili kuhakikisha kwamba, ujumbe na kweli za Kiinjili zinawafikia watu wengi zaidi, hususan maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hata hawa wanayo shahuku ya kutaka kumsikia na kumwona Yesu Kristo kwa njia ya Maandiko Matakatifu, Mafundisho ya Kanisa, Sala na shuhuda za imani tendaji.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii ni changamoto lakini pia ni fursa makini kwa maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millennia ya tatu ya Ukristo, Mama Kanisa anapojikita katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, ili kuwatangazia Watu wa Mataifa upendo na huruma ya Mungu inayomwokoa mwanadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoogopa kutumia mitandao ya kijamii, licha ya matatizo na changamoto mbali mbali zilizopo, lakini wanapaswa kushuhudia kile wanacho amini kama njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Kanisa haliwezi kuwatwishwa watu mizigo kwa mafuriko ya habari, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, maneno haya yanakwenda sanjari na ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha.

Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa ni Mama na Mwalimu. Watu wa nyakati hizi wanapenda kuona ushuhuda, kwani “wamechoka na longolongo kibao”. Matendo ya mtu ni mwalimu tosha kabisa. Kanisa litaendelea kufanyia kazi changamoto na matatizo yanayojitokeza katika njia za mawasiliano ya kijamii, ili kweli Kanisa pia liweze kumtangaza Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu kwa njia ya ulimwengu wa digitali, unaovuma kwa wakati huu.

Askofu mkuu Claudio Maria Celli, anayaalika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Majimbo, Parokia na Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, kuhakikisha kwamba, yanafanya maboresho mara kwa mara katika mitandao yao, ili kuwavutia watu kutembelea huko. Ni kweli kwamba, si kila Jimbo wala Parokia ina mtandao wa kijamii, lakini pia Familia ya Mungu inapaswa kusoma alama za nyakati kwa kujibidisha kuendeleza njia za mawasiliano kadiri ya uwezo na fursa zilizopo, ili kukoleza mchakato wa watu kukutana na kujadiliana.

Ikumbukwe kwamba, Familia ya Mungu inapaswa kukutana kama: Jumuiya ya Waamini, kama zilivyo Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, ili kujadili na kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Waamini wakutane katika maadhimisho ya Ibadan a Liturujia mbali mbali ili kulishwa kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, tayari kuwashuhudia walimwengu kwamba, wao kweli wamekutana na Yesu Kristo Mfufuka. Askofu mkuu Celli anasema kwamba, wafanyakazi na wadau mbali mbali katika sekta ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwa kweli ni vyombo vya ukweli, haki na amani kwa kuzingatia kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu. Wasimame kidete kumlinda na kumwendeleza mwanadamu ili aweze kufikia ukomavu katika maisha na wito wake hapa duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waandishi wa habari kuwa kweli ni wahudumu na vyombo vya ukweli, wema na uzuri, kwa kusimama kidete kutetea kile kilicho chema, kizuri na kitakatifu, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu. Mawasiliano hayana budi kuwa ni chombo cha ukweli, wema na uzuri anasema Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la mawasiliano ya jamii katika mahojiano maalum na wakala wa habari, Zenit.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.