2015-12-24 08:15:00

Onesheni ujasiri kwa kujenga amani inayojikita katika haki na usalama!


Patriaki Fouad Twal wa Yerusalemu katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2015 kwa namna ya pekee kabisa anaombea amani na usalama kwa Waisraeli na wapelstina. Anapenda kuona vita, kinzani na migogoro sehemu mbali mbali ya dunia inapata suluhu kwa njia ya majadiliano, ili haki, amani na maridhiano kati ya watu yaweze kutawala katika akili na mioyo ya watu. Hiki ni kipindi cha kuonesha ujasiri ili kujenga amani inayojikita katika haki.

Viongozi wa Israeli na Palestina wanapaswa kuheshimu na kuzingatia makubaliano ya kimataifa kwa kuambata mafao ya wengi huko Mashariki ya Kati. Utu, heshima na usalama wa maisha ya watu na mali zao ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha haki na amani. Patriaki Twal katika ujumbe wake anakaza kusema, mashambulizi ya kigaidi yaliyojitokeza hivi karibuni sehemu mbali mbali za dunia yanawajengea watu hofu na mashaka. Huko Mashariki ya kati kuna vita inayoendelea kupamba moto. Haya ni matokeo ya biashara haramu ya silaha inayokumbatia utajiri na faida kubwa kwa kubeza maisha ya watu na mali zao.

Wafanyabiashara hii wanaalikwa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kukumbatia Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo. Wafanyabiashara haramu ya silaha watambue kwamba, wanayo kesi ya kujibu mbele ya Mungu kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Vita na mashambulizi ya silaha kamwe hayataweza kutatua shida na changamoto zinazomwandama binadamu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, umaskini unavaliwa njuga hadi kupewa kisogo kwani umaskini na ukosefu wa haki msingi ni mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kushamiri kwa vitendo vya kigaidi.

Kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, kiwe ni kipindi muafaka cha kufanya maamuzi magumu katika maisha, kwa kumwongokea Mungu, ili kuuvua utu wa kale tayari kumwambata Kristo Yesu. Waamini wanahamasishwa kuondokana na ubinafsi na badala yake kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ndani ya jamii.

Wanasiasa watambue kwamba, huruma ya Mungu ni sehemu ya vinasaba na maisha ya kisiasa kwa kutambua kuwa siasa ni kwa ajili ya huduma na maendeleo ya wengi. Wanasiasa wanapaswa kuwa ni mfano bora wa tunu msingi za maisha ya kiutu, kifamilia, kimaadili na kitamaduni kwa kuambata huruma ya Mungu. Kwa njia hii wanasiasa wanaweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, upendo, upatanisho na maridhiano ya kijamii.

Patriaki Fouad Twal anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kuwa na kiasi na Parokia zote kuhakikisha kwamba, zinasali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wahanga wa vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Kutokana na hali ngumu ya maisha na mazingira tata, waamini watumie kipindi cha Noeli kutafakari kuhusu umuhimu wa Noeli katika maisha yao ya kiroho, kwa kuonesha mshikamano na watu wanaoteseka kutokana na mashambulizi ya kigaidi. Siku kuu ya Noeli iguse akili na mioyo ya waamini badala ya kuendekeza mambo ya nje, anasa na starehe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.