2015-12-24 08:46:00

Onesheni huruma kwa wakimbizi na wahamiaji: Noeli ni kipindi cha matumaini


Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, Lwf , katika ujumbe wake wa Kipindi cha Noeli linasema kwamba, huu ni muda wa matumaini unaojikita kwa namna ya pekee katika mchakato wa upendo na ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotafuta usalama na ubora wa maisha. Kuna mamillioni ya watu wanaokimbia nchi zao kutokana na vita, kinzani, mipasuko ya kijamii; dhuluma na nyanyaso za kidini bila kusahau majanga asilia.

Waamini watambue kwamba, katika sura na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji, hapo wanaiona sura ya Kristo mteswa pamoja na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu anasema Askofu Munib A. Younan, Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani. Hii ni tafakari inayotolewa na kiongozi ambaye ameonja machungu na adha ya wakimbizi huko Yordani na Nchi Takatifu. Lakini anakumbusha pia kwamba, familia yake, kunako mwaka 1948 ilibidi kukimbilia uhamishoni kutokana na Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Noeli, iwe ni fursa kwa waamini kuguswa na ukarimu kutoka katika undani wa maisha yao kwa kumwangalia na kumtafakari Neno wa Mungu aliyefanyika mwili katika hali ya unyonge na unyenyekevu mkuu. Watu watambue kwamba, dunia mamboleo ina kiu ya kuona haki, amani, usalama na maridhiano yanatawala katika maisha ya watu. Vita, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini huko Mashariki ya Kati, Asia na Afrika; Marekani na Ulaya ziwakumbushe waamini mateso yaliyowakumba Maria na Yosefu kwa kukosa mahali pa kujihifadhi kiasi cha kukimbilia Pangoni, mahali pa kulishia wanyama!

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujiuliza swali la msingi ikiwa kama ulimwengu mamboleo unayo nafasi kwa zawadi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kumbe, Kipindi cha Noeli ni wakati muafaka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuwa kweli ni wajumbe wa haki, amani na maridhiano kati ya watu waliokata tamaa! Hawa ndio wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliochoka na kuelemewa na magumu ya maisha.

Waamini wa Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani wanaalikwa kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ujumbe huu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa ajili ya kuwasaidia kwa hali na mali wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Waamini wawe na huruma kwa wakimbizi na wahamiaji ambao idadi yao inazidi kuongezeka maradufu duniani. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, mwishoni mwa mwaka 2014 kumekuwepo na wakimbizi zaidi ya millioni 59. 5. Hawa ni watu wanaohitaji kuonjeshwa huruma na upendo unaobubujika kutoka katika ushuhuda wa maisha ya Wakristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.