2015-12-24 16:52:00

Noeli ni Siku kuu ya akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi!


Kwa kawaida wakati wa kusoma matokeo ya uchaguzi wa viongozi, msomaji huanza kusoma jina la aliyepata kura chache kupita wote hadi kwa mshindi aliyechaguliwa kwa kura nyingi zaidi. Kwa vyovyote kutokana na mwendo wa kampeni zilivyofanyika wapiga kura wanaweza kubunia mshindi atakuwa nani. Leo tutamshuhudia mshindi aliyepata kura zote licha ya wingi wa ushabiki wakati wa kampeni. Tunamshuhudia mtangazaji wa matokeo na wapambe watakaoshangilia ushindi.

Tuanze kwa kuona mchanganuo wa makundi ya wakandidati waliopigiwa kura. Katika mchanganuo huo, tutaongozwa na fasuli ya Injili ya leo. Mwinjili Luka anatutambulisha makundi mawili tofauti ya wagombea uchaguzi. Mosi ni watu wanyonge, akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi;  na wanyamugi wa mwisho; walala pu! Hawa wakiwa ni mzee Zakaria, halafu bibi kizee Elizabeti aliye tasa toka kuzaliwa, anafuata msichana mdogo kabisa wa miaka yapata kumi na nne kutoka Nazareti anaitwa Maria mja mzito na mchumba wake Yosefu kijana wa miaka kumi na nane hivi. Kundi hili la watu halina thamani yoyote ile katika jamii.

Pili, kuna vigogo wa ulimwenguni walioishajitangazia ushindi wakala na kushiba, wakasahau kwamba, mbeleni kuna kifo chaja! Wa kwanza kabisa ni Kaisari Augusto. Alama yake kubwa ni kuhesabu watu. “Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu.” Huyu alikuwa mtawala mwenye mamlaka na hadhi kama ya miungu wadogo. Alitawala ulimwengu mzima na anaitisha sensa ya watu ulimwengu mzima wa wakati wake. Sensa iliyomsaidia kujua idadi ya raia wanaoweza kukusanya kodi ya kichwa na ya mapato, na idadi anayoweza kuunda jeshi la kupigania utawala wake.

Kigogo wa pili katika kundi hili la wakuu ndiye Kirenio wa Siria. Mwinjili anatujulisha kuwa sensa hiyo ilikuwa ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu – Siria.  Hili lilikuwa ni taifa la nchi jirani ya Waisraeli lililokuwa chini ya himaya ya Augusto wa Roma. Kwa hiyo utawala na mamlaka aliyokuwa nayo Augusto yaliendea sana, ndiyo maana anaagiza kufanya orodha ya ulimwengu mzima. Wakuu wa nchi walipokuwa wanafanya sensa, raia wao iliwabidi kuinama vichwa kuonesha kukubali kuhesabiwa na kutawaliwa. Kwa hiyo watawala wa ulimwengu wanafanya watu kuinamisha vichwa na kutawala.

Lakini haina budi ieleweke kwamba kwa Wayahudi, ni Mungu peke yake ni mwenye mamlaka na haki ya kuhesabu watu. Sensa ya Mungu inajulikana kuwa ni “Kuinua kichwa.” Watu wengine wanaoingia katika kundi lile la kwanza, lakini hili ni la watu chukivu kabisa ni la wachungaji. Kadiri ya utamaduni wa Wayahudi watu hawa walilaaniwa sana na jamii, waliogopwa na kudharaulika. Walijulikana kuwa ni wabaya wevi na watu wa mataifa wasioaminika. Hawakuruhusiwa hata kuingia Hekaluni kusali. Hivi hata shughuli zao za kuchunga walifanya gizani usiku wakiogopa kuonekana kwenye mwanga wa jua la mchana. Walipenda giza kwa sababu mwanga utaumbua uovu wao na ubaya wao.

Baada ya kuona makundi haya sasa tuone mchakato mzima wa mambo ulivyokuwa. Pindi Maria na Yosefu wako huko Betlehemu walikoenda kuhesabiwa, muda wa Maria kuzaa ulikuwa umefika, Maria akamzaa mtoto. Tena yasemwa kuwa “hakukuwa pahala katika nyumba ya kulala.”  Yaonekana kama vile safari hii walishtukizwa au walifukuzwa. Tafsiri hii inadhalilisha watu wa Mashariki. Kutokana na ukarimu wa Wayahudi isingewezekana familia hii ikose mahali pa kukaa. Isipokuwa walikosa mahala pa kujisetiri kwa mama anayekaribia kujifungua. Aidha, safari hii ilipangwa tena walifika hapo siku mbili kabla kwani imesemwa “pindi wakiwa huko.”

Halafu “Maria alimzaa Mwana wake wa kwanza.” Hapa tena suala la mtoto wa kwanza linakanganya wengi. Yaonekana kama vile Maria alikuwa na watoto wengine tena baadaye. La hasha bali kadiri ya utamaduni wa Wayahudi, wao walikuwa na utaratibu wa kumtia wakfu mtoto wa kwanza, maana yake kumtolea kwa Mungu kwa ajili ya mambo yanayomhusu Mungu. Kwa hiyo Maria anamzaa mtoto wake wa kwanza yaani anamtolea – wakfu – kwa Mungu. Hapa akina mama wote wanafundishwa kuwaacha mtoto wao wafanye kile anachowatakia Mungu, yaani kumwachia Mungu atimize lengo lake juu ya watoto wao.

Kisha Maria “akamviringishwa vitambaa” ili kuonesha kuwa mtoto huyu ni mtu kama watu wengine. Kwa hiyo kama asingekufa msalabani angekufa kwa uzee.  Halafu tena “Maria akamlaza kwenye hori” Isaya mwanzoni anasema, “watu wa Israeli hawamfahamu Bwana wao kumbe ngombe na  punda wanatambua hori la Bwana wao.” Maana yake, sisi tunaalikwa kumtambua Bwana wetu aliyezaliwa katika hali nyonge, kwa ajili ya wanyonge ili kuwakomboa katika hali hii tayari kuambata huruma, upendo na baraka za Mungu.

 Baada ya Maria kujifungua mtoto mchanga na kumlaza horini, kunaingia suala la kumpigia kura. Kundi la kwanza la watu wanyonge ndiyo wasimamizi wa kura, yaani Yosefu na Maria. Tungetegemea kundi la vigogo lingekuwa la pili kuja kumpigia kura ya kumfuata kigogo mwenzao. Lakini kutokana na jinsi alivyofanya kampeni yake, na hali anayoonesha pale alipolala, vigogo hao hawajitokezi. Kundi pekee llinalojitokeza ni la Wachungaji waliokuwa katika usiku wa giza. Wanatokewa na malaika na kupashwa habari ya kwenda kupiga kura mchana.

Malaika wanawaambia “Ninawaletea habari njema ya furaha kuu. Amezaliwa kwa ajili yenu katika mji wa Daudi mwokozi, Kristo Bwana. Hii ni alama, mtamkuta mtoto amefunika mavazi na kulazwa kwenye hori la kulishia manyama.” Wachungaji wanashtuka na kushangaa, kwamba hata wao wametazamwa. Kwamba wamechaguliwa kumpigia kura Masiha. Wanapata ushindi pale wapoondoka kwenda kumwangalia mtoto. Huyu ni mtoto wa kawaida kabisa amezaliwa katika mazingira ya kimaskini kwa ajili ya maskini na waovu wote. Jeshi lake siyo la askari wenye silaha za kutisha kwa ajili kuwalinda watawala wa ulimwengu, bali ni la Malaika.

Hawa ndiyo wapambe, wanaofurahia mshindi, yaani wanyonge waliopata kura nyingi, wamechaguliwa na Mungu kuwa wa kwanza. Malaika hao wanaimba kwa furaha kuwashangilia hao waliochaguliwa na mnyonge mwenzao. Hivi wanawashangilia wanyonge kwa wimbo huu: “utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu anaowapenda.” Siyo na “ kwa watu wenye mapenzi mema,” kwani amani ni kwa wanyonge, wadhambi, waovu hao ndiyo walioshinda uchaguzi kwa sababu Mungu amewapenda hao zaidi zaidi  kuliko watawala. Upendo wa Mungu umewashukia wanyonge na watu kama hao. Heri kwa Sikukuu ya Noeli.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.