2015-12-23 11:49:00

Vatican inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 tangu ilipoanza kutumia mitandao


Monsinyo Lucio Adrian Ruiz, katibu mkuu wa Sekretarieti ya mawasiliano na mkuu wa idara ya mitandao ya kijamii mjini Vatican anasema, ilikuwa ni tarehe 25 Desemba 1995, miaka ishirini iliyopita, Mtakatifu Yohane Paulo II alipozindua mtandao wa Vatican na huo ukawa ni mwanzo wa matumizi ya mtandao hapa mjini Vatican, huduma ambayo imekuwa ni msaada mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Vatican. Leo hii kuna maelfu ya watu wanaoogelea kwenye mtandao wa Vatican wakitafuta habari kuhusu maisha na utume wa Kanisa, jambo la kumshukuru Mungu.

Monsinyo Ruiz anasema, huu ulikuwa ni mwanzo na mang’amuzi mapya, mwelekeo wa kinabii uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetaka kuhakikisha kwamba, hata Kanisa linaendelea kusoma alama za nyakati wa kutumia mitandao ya kijamii, ili kuwatangazia Watu wa Mataifa, Habari Njema ya Wokovu. Tarehe 25 Desemba 1995, Siku kuu ya Noeli pamoja na kuzaliwa kwa mtandao wa Vatican, kunaonesha kwa namna ya pekee, jinsi ambavyo utamaduni unatembea na kuandama historia ya maisha ya mwanadamu!

Kwa mara ya kwanza, Mtakatifu Yohane Paulo II alianza kwa kutoa Ujumbe wa Noeli kwa mwaka 1995 “Urbi et Orbi”, tangu wakati huo, Kanisa limeendelea kusoma alama za nyakati kwa kuhakikisha kwamba, linaendelea kutumia kwa uhakika maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mchakato wa Uinjilishaji mpya pamoja na kuwajuza walimwengu kuhusu maisha na utume wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II katika wosia wake anakaza kusema, Kanisa halina budi kuendelea kusoma alama za nyakati kwa kuhakikisha kwamba, linatumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari kwa ajili ya utume na maisha yake.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, hakuna sababu ya kuogopa maendeleo ya sayansi na teknolojia, bali Kanisa lisimame kidete kuhakikisha kwamba, linayatumia kikamilifu, kwa hekima na busara. Huu ndio mwelekeo unaotolewa pia na Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa, kwenda pembezoni mwa jamii, kwa kuzingatia mambo msingi; tayari kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana. Mawasiliano katika mtindo wa digitali unaliwezesha Kanisa kukutana na vijana, huko kwenye viunga vyao, walikobana, tayari kuwashirikisha utume na maisha ya Kanisa. Kumbe, changamoto kwa Kanisa kwa wakati huu, ni kutoka na kuwaendea watu!

Matumizi ya mitandao ya kijamii anasema Monsinyo Lucio Adrian Ruiz yana changamoto zake, kwani hapa watumiaji wa mitandao wanakutana kama binadamu na wala si kama mashine. Hapa ni mahali pa watu kushirikishana habari, picha na maneno. Hapa pia ni fursa nzuri ya kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani hususan wakati huu Mama Kanisa anpoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huduma za kichungaji, moyo wa huruma na upendo, ni mambo ambayo hayana budi kumwlishwa hata kwenye mitandao ya kijamii. Watu waonje huruma ya Mungu, wasaidiwe kuboresha na kupyaisha maisha yao ya kiroho.

Mitandao ya kijamii ikitumika kwa hekima na busara, inaweza kuwa kweli ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa watu wa nyakati hizi. Hapa watu wanaweza kujenga mshikamano wa upendo, kwa kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama kielelezo cha imani tendaji. Mitandao ya kijamii inaweza kuwa ni mahali pa kuikutanisha Familia ya binadamu na kwa wakristo hapa wanaweza kuonjeshana imani, upendo, huruma na matumaini hadi miisho ya dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.