2015-12-23 10:37:00

Onesheni mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji!


Inashangaza kuona kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni watoto wengi wamelazimika kuwa ni wakimbizi na wahamiaji, kutokana na kufuatana na wazazi wao, wanaokimbia nchi zao, ili kutafuta usalama na maisha bora zaidi. Hawa ni watu wanaoendelea kuteseka na kunyanyasika na kwamba, idadi ya watoto wakimbizi na wahamiaji wanaokufa maji huko Baharini inaendelea kuongezeka maradufu. Kutokana na changamoto hii kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wa umoja na udugu, ili kuweza kukabiliana na changamoto hii inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Kuna sababu mbali mbali zinazowafanya watu wengi kukimbia nchi zao, lakini kwa sasa kubwa zaidi ni nyanyaso na dhuluma za kidini. Hivi ndivyo anavyosema Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2015. Kanisa hili linaendelea kufuatia kwa umakini makundi makubwa ya wakimbizi yanayotafuta hifadhi ya maisha. Ni kweli kwamba, katika historia ya maisha ya binadamu kumekuwepo na wimbi la wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hususan wakati wa Vita kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia.

Viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii wakaibuka na matamko ya amani na maridhiano ya kati ya watu, hali ambayo ingetegemewa kwamba, ingewasaidia watu kuishi kwa haki, amani na naridhiano, lakini kwa bahati mbaya, matumaini ya watu wengi yameingia “mchanga” kutokana ukweli kwamba, nyakati hizi, Jumuiya ya Kimataifa inashuhudia makundi makubwa ya wahamiaji na wakimbizi yakirandaranda sehemu mbali mbali za dunia, kutafuta usalama na maisha bora zaidi.

Changamoto hii inapaswa kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuwajibika zaidi na kwamba, haiwezekani kwa watu kukaa kitako na kufumbia macho mateso, shida na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Makundi haya yanapaswa kuonjeshwa mshikamano wa upendo, kwa kutambua na kuthamini uso wa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo ambaye kwa namna ya pekee kabisa amejifunua kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya watu wake!

Huyu ndiye Yesu Kristo ambaye amekuja duniani si kama: Mfalme, Mtawala au Tajiri, bali kama Mtoto aliyezaliwa kwenye Pango la kulishia wanyama, baada ya kukosa mahali pa salama. Hii ndiyo hali wanayokumbana nayo wahamiaji na wakimbizi sehemu mbali mbali za dunia anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza. Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ililazimika kukimbilia uhamishoni, ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu yaliyokuwa hatarini kutokana na chuki iliyooneshwa na Mfalme Herode!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anahitimisha ujumbe wake wa Noeli kwa mwaka 2015 kwa masikitiko makubwa kwamba, kuna watu wanaoendelea kupoteza maisha yao huko baharini na jangwani; hawa ni watoto na watu wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha; kutoka na chuki na wasi wasi mkubwa, Misri ikatoa hifadhi kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Hii ni changamoto kwa Waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko, dhuluma na nyanyaso za wakimbizi na wahamiaji, bila kuangalia rangi, dini au mahali anapotoka mtu, wote wanahitaji kuonjeshwa mshikamano wa huruma na mapendo! Kwa njia hii, kweli Noeli inaweza kupata maana na mwelekeo mpya kwa Mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.