2015-12-23 09:48:00

Mheshimiwa Padre Justin Mulenga ateuliwa kuwa Askofu mpya wa Mpika, Zambia


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa sana Padre Justin Mulenga kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Mpika, Zambia, kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule alikuwa ni Mratibu wa shughuli za kichungaji, Jimbo kuu la Kasama, Zambia. Askofu mteule Mulenga alizaliwa tarehe 27 Februari 1955 Parokiani Nondo, Jimbo kuu la Kasama. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja takatifu la Upadre hapo tarehe 18 Julai 1993.

Katika maisha na utume wake wa Kikuhani, amewahi kuwa Paroko msaidizi, Mchumi wa Jimbo kuu la Kasama; Paroko wa Kanisa kuu la Mtakatifu John, Jimbo kuu la Kasama na St. Francis, sanjari na kuwa Makamu Askofu upande wa Watawa Jimbo kuu la Kasama pamoja na kuwa ni Dekano wa Mbala. Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Mpika limekuwa wazi tangu tarehe 12 Januari 2012, baada ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kumteuwa Askofu Ignatius Chama kuwa Askofu mkuu wa Jimbo Katoliki Kasama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.