2015-12-22 09:43:00

Wasaidieni waamini kujiandaa kikamilifu kuadhimisha Fumbo la Huruma ya Mungu!


Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume katika barua yake kwa waungamishaji wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, anawaalika kujiandaa kikamilifu katika kuliadhimisha Fumbo la Familia Takatifu, ambalo kwalo, Mwana wa Baba wa Milele, aliamua kujifanya mwanadamu kwa ajili ya binadamu, ili aweze kumjalia wokovu na maondoleo ya dhambi. Noeli ni Siku kuu ambayo inawakumbusha waamini kwa namna ya pekee, Fumbo la Huruma ya Mungu.

Kardinali Piacenza anasema, Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, atazingatia ukweli unaofumbatwa upendo kwa jirani; upendo ambao unatekelezwa kwa akili na uhuru kamili; upendo usiomilili, bali unaotambua na kuambata kile kilicho chema na kitakatifu; upendo unaomchangamotisha mwamini kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani zake, badala ya kuwanyonya. Huu ni upendo unaobubujika kutoka katika uelewa makini wa Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipofanyika mwili na kukaa kati ya watu wake.

Yesu Kristo kwa mara ya kwanza alikuja na kuzaliwa mjini Bethlehemu na kwa wakati huu anaendelea kujionesha kwa njia ya Mafumbo ya Kanisa na nyakati za mwisho, atakuja kwa utukufu ili kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Waamini wanahamasishwa kukuza na kudumisha upendo wao kwa Kristo kwa kutambua kwamba, huu ni upendo ambao “umechakachuliwa” kwa dhambi. Kumbe, unapaswa kutakaswa na kuokolewa kwa njia ya neema inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Yesu ni kiini cha Fumbo la Huruma ya Mungu, anayeweza kutakasa pendo la kibinadamu, kwani Kristo ni Hakimu na Mkombozi; Ni Haki, Upendo na Huruma ya Mungu. Ukuu, huruma na upendo wa Mungu unajidhihirisha kwa namna ya pekee kabisa katika Sakramenti ya Upatanisho, mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanakimbilia huruma na upendo wa Mungu, kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.

Mwamini aliyetubu na kuungama vyema dhambi zake, anakutana na Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kumbe, waamini wakitambua ukweli huu wa imani, wanaweza kuwa wepesi kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, kwa kujiweka wazi mbele ya Ukweli wa Fumbo la Kristo na Huruma ya Mungu. Hapo mdhambi anajisikia kukumbatiwa na kuondolewa dhambi zake pamoja na kupewa mageuzi katika maisha, tayari kumuiga, kumwona na kumshudia kwa njia ya furaha inayomwilishwa katika imani tendaji.

Kardinali Mauro Piacenza anawaalika Mapadre waungamishaji kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma hii makini, ili kuwasaidia waamini kukutana na Fumbo la Ukweli na Huruma ya Mungu katika maisha yao; ili katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, waamini waweze kweli kumwona na kumshuhudia Mtoto Yesu anayelala Pangoni mwa kulishia wanyama kule Bethlehemu. Wawe na ujasiri wa kuwasaidia waamini kuanza maisha mapya, kwa kuambata huruma na upendo wa Mungu. Waamini wajenge utamaduni wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili waweze kusafisha dhambi zao, ili waweze kuwa safi na weupe kama theluji!

Kardinali Mauro Piacenza anawaalika waungamishaji kusindikizana kwa njia ya sala na sadaka zao, ili kuwasaidia waamini kuweza kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho. Hii ni huduma inayopaswa kutekelezwa kwa uvumilivu mkubwa na upendo wa kichungaji kwa ajili ya kuendelea kulipyaisha Kanisa la Kristo. Kila Padre ahakikishe kwamba, anaimarisha imani na kuendelea kuwa mwaminifu kwa wito na maisha yake ya Kikasisi, daima akiambata toba na wongofu wa ndani, ili aweze kuwa kweli ni mhudumu wa Fumbo la Huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.